Alfajiri ya Alhamisi wakati taifa lilipokuwa linajiandaa kusherehekea mashujaa wa taifa miaka 60 tangu uhuru, wakili aliyekuwa uhamishoni, Miguna Miguna naye aliwasili baada ya takribani miaka 5 akiwa amezuiliwa kurudi nyumbani.
Katika mazungumzo yake ya kwanza na wanahabari katika anga tua ya JKIA, Miguna aliwamiminia Wakenya sifa tele kwa kuonyesha uzalendo na kumpigani kurudi nchini, dhidi ya vizuizi vilivyokuwa vimewekwa dhidi yake na serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Miguna aliwapongeza Wakenya kwa kumpigia rais Ruto kura kwa wingi na kuhakikisha ushindi wake katika kile alisema kwamba pasi na uongozi wa hii serikali ya Ruto basi hata yeye hangeweza kuruhusiwa kusafiri kuja nchini kutokana na vizuizi vingi vilivyolimbikizwa dhidi yake.
“Nina furaha kubwa sana kurudi nyumbani. Narudisha shukrani zangu kwa Wakenya ambao wamesimama na mimi na pia kwa kumpigia kura kwa wingi rais William Ruto kwa sababu ushindi wake ni wa maana kwangu. Pasi na uongozi wa Kenya Kwanza mimi nisingerudi nyumbani,” Miguna alisema.
Jenerali huyo wa kujitangaza mwenyewe alifichua kwamba amepokea mwaliko wa kuhudhuria sherehe za Mashujaa zitakazofanyika katika uwanja wa kijeshi ulioko Lang’ata jijini Nairobi.
Kandi na kuhudhuria sherehe hizo, Miguna pia alidokeza kwamba ratiba ya siku yake itakamilikia katika ikulu ya Nairobi ambapo pia amepokea mwaliko wa kukutana na rais William Ruto baadae mchana.