Mbunge wa Embakasi East Babu Owino kama kawaida yake kwa mara nyingine tena aliwazuzua wabunge kwa Kishwahili chake kilichojawa na utashi ainati.
Mbunge huyo ambaye alikuwa anajibu madai ya mbunge mmoja aliyemtaja kama mmoja wa wabunge ambao wanapata ugumu katika kujieleza kwa lugha ya Kiswahili alisimama na kulainisha mambo huku akijidai kwamba weledi wake katika lugha hiyo inayofagiliwa sawa ukanda wa Afrika Mashariki ni wa kiwango kilichotukuka.
Aliamua kudhibitisha si tu kwa maneno bali pia katika vitendo aliposimama na kuanza kutema hoja katika lugha ya Kiswahili ila akatumia maneno yanayokinzana si tu katika sintakisia bali pia katika mtiririko wa kimawazo na kinadharia huku wabunge wenzake wakishindwa kujizuia kwa vicheko.
“Bwana Spika tumesikia mheshimiwa Pukose amenitaja ya kuwa mimi huongea tu mambo ya Sheng’, ile lugha ambayo si ya kueleweka. Bwana spika nataka kukuambia kwamba leo hii nimejawa na bashasha mpwekwempwekwe chakari ja kunguni. Maanake tunatukuza Kiswahili bwana spika,” Owino alisema huku akikatizwa kwa kicheko cha Wabunge wenza.
Alizidi kutamba akisema kwamba wabunge wengi waliokuwa wakicheka hawakuwa na ufahamu wa kile alichokisema kutokana na kutoelewa Kiswahili. Aliwataka wabunge wenza kurudi shule wasome lugha ya Kiswahili.
Mjadala huu ulikuwa bungeni ambapo baadhi ya wabunge walitaka mswada upitishwe bungeni kuunda kamati inayoshughulikia masuala ya lugha ya Kiswahili ambayo wengi walihisi kwamba haipewi uzito unaofaa.