Daktari katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta amewaonya wakazi wa Nairobi kuhusu visa vingi vya kuchomwa visu katika jiji hilo katika chapisho ambalo limesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Bi Lilian Munyua alibaini kuwa ameshuhudia ongezeko la waathiriwa wa kudungwa kisu wakikimbizwa hospitalini, akidai wiki mbili zilizopita hazikuwa rahisi kwake kazini.
“Ikiwa una familia au marafiki wa karibu wanaokuja Nairobi au wanaoishi hapa, tafadhali washauri ipasavyo. Wiki hizi mbili zilizopita hazijakuwa rahisi kazini. Tunapokea wastani wa kesi 4 - 7 za kuchomwa visu kila siku kutoka kwa wahuni karibu na jiji. Nimewatazama vijana kwa wazee bila msaada, wanaume kwa wanawake, wakikata roho huku nikijaribu kuwaokoa. Wengine wako ICU huku wengine wamenusurika lakini wakiwa na majeraha ya maisha,” Dkt Munyua aliandika kwenye Facebook yake.
Aliendelea kufichua baadhi ya maeneo ambapo waathiriwa wa visa vya dharura vya kuchomwa visu wanapokea hospitalini mara nyingi hutokea.
“Kesi nyingi kati ya hizi zinatoka;
✅ Flyover ya kuelekea KCA
✅ KCA Underpass & Total Exit
✅ Globe Roundabout na Barabara ya Kipande
✅ ABC na Kangemi kando ya Njia ya Waiyaki.
✅ Naivas AllSops kando ya Thika Super Highway
✅ CBD (Archives), River Road, Fig Tree, karibu na Ofisi za KBC nk.”
Daktari huyo katika chapisho hilo ambalo sasa liesambaa pakubwa alizidi kuelezea kwamba wahuni hao wanatekeleza visa hivyo mchana peupe ambapo mtu akikataa kutii amri yao wanamchoma visu.
“Washauri marafiki na familia yako kuepuka kutembea peke yao au kuchelewa katika maeneo haya. Ikiwa umebeba kompyuta ya mkononi kwenye mkoba, unasalia kuwa mlengwa wao, hakikisha kwamba utaipoteza au kupoteza maisha yako katika maeneo haya,” Dkt Munyua alisema.