Mwanamume achomwa kisu hadi kufa katika baa Kitengela

Polisi walisema mshukiwa alifunga baa mara moja na kutoroka eneo la tukio.

Muhtasari
  • Alisema mshukiwa huyo anafuatiliwa na ilikuwa ni suala la muda kabla ya kukamatwa kwake
  • Mshukiwa huyo kulingana na habari ameolewa na ana familia changa
  • Maafisa wakuu wa polisi Alhamisi walitembelea kituo cha polisi cha Kitengela kuhusiana na kisa hicho
Crime Scene

urugenzi ya Upelelezi wa Jinai inachunguza kisa ambapo mwanamume mmoja alidaiwa kuuawa kwa kudungwa kisu katika baa moja  Kitengela, kaunti ya Kajiado.

Hussein Fuad Abdow, 26, alitangazwa kufariki alipofika katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kitengela Level 4 ambapo alikuwa amekimbizwa baada ya kisa cha Jumanne saa 7.10 jioni.

Duru za polisi zilisema kwamba Abdow alivamiwa na mmiliki wa baa hiyo iliyoko eneo la G26 la Kitengela.

Mshukiwa ana baa huko Kitengela ambako alikuwa ameajiri mwanamke mwenye asili ya Ethiopia kama mhudumu," afisa mmoja aliyefahamu kisa hicho alisema Alhamisi.

"Inaaminika kuwa marehemu alikuwa akimtembelea mwanamke huyo kwenye baa, mahali pake pa kazi, lakini mwajiri hakufurahi."

Alisema marehemu alikuwa ameonywa mara kadhaa kuhusu kumuona mwanamke huyo lakini hakusikiliza.

“Marehemu jana alitembelea baa hiyo lakini akamkuta mwanaume huyo. Kulingana na shahidi makabiliano yalitokea kati ya wawili hao na kusababisha marehemu kudungwa kwa kisu,” polisi walisema.

Abdow ambaye kulingana na polisi aliishi Sabaki, kaunti ya Machakos alikuwa na rafiki yake wakati wa kisa hicho. Rafiki huyo ni miongoni mwa mashahidi katika kesi hiyo.

Alikimbizwa hospitali na daktari katika hospitali hiyo alifahamisha maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kitengela kuhusu kifo chake.

Maafisa wakuu wa polisi katika kituo hicho walikimbilia hospitalini na kubaini kuwa marehemu alikuwa na jeraha moja la kisu upande wa nyuma wa kulia.

Polisi walisema mshukiwa alifunga baa mara moja na kutoroka eneo la tukio.

“Mshukiwa yuko huru. Alitoroka kabla ya marehemu kukimbizwa hospitalini,” afisa wa upelelezi alisema.

Alisema mshukiwa huyo anafuatiliwa na ilikuwa ni suala la muda kabla ya kukamatwa kwake.

Mshukiwa huyo kulingana na habari ameolewa na ana familia changa.

Maafisa wakuu wa polisi Alhamisi walitembelea kituo cha polisi cha Kitengela kuhusiana na kisa hicho.

Hata hivyo, habari za polisi zilisema kiwango cha uhalifu katika mji huo kilipungua baada ya majambazi kadhaa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Washukiwa tisa wa ujambazi wanaohusishwa na visa vingi vya uhalifu huko Kitengela na viunga vyake hivi majuzi walikamatwa na kufikishwa katika mahakama kuu ya Kajiado.

Tangu wakati huo wamewekwa rumande.

Vitu kadhaa vilivyoibiwa vilipatikana kutoka kwa washukiwa vimetambuliwa vyema na walalamishi husika.