Wakaazi wa Ruaka eneo la Kiambu, waligutushwa na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 5 lilokuwa likijengwa.
Jengo hili ambalo limeanguka karibu na eneo ya Fortune Club liliangukia nyumba zingine za karibu.
Kulingana na ripoti za awali mtu mmoja aliokolewa kwenye jengo hilo huku waokoaji wakiendelea kufukua vifusi vya jengo hilo. Kuna hofu kuwa huenda kuna watu waliokwama ndani ya jengo hilo.
Maafisa wa uokoaji kutoka kaunti ya Kiambu, msalaba mwekundu na idara ya polisi tayari wamefika kwenye eneo la tukio.
Huo ni mkasa wa pili kutokea chini ya wiki moja baada ya jengo la ghorofa 7 kuanguka eneo la Seasons,Kasarani siku ya Jumanne Novemba 14.
Takriban watu 3 walikufa wakati jengo hilo lilipoporomoka. Watu wengine 6 waliokolewa kutoka kwa vifusi.