logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanaume akamatwa Nairobi akimiliki simu 265 za Iphone na 10 za Android

Kukamatwa kwake kunakuja wiki moja baada ya waziri Kindiki kutoa onyo kali dhidi ya magenge wa ujambazi.

image
na Davis Ojiambo

Habari22 November 2022 - 09:50

Muhtasari


  • •  "Vitu hivyo vinashukiwa kuibiwa kutoka kwa umma," ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyofichuliwa kwa vyombo vya habari.
Simu kadhaa zilizokamatwa kutoka kwa mshukiwa

Jumatatu polisi jijini Nairobi walimtia mbaroni mwanaume mmoja,29, mshukiwa wa uharifu kwa kumiliki simu aina ya Iphone zitapazo 265 katika mtaa wa Kasarani. Mwanaume huyo pia alipatikana na simu 10 aina ya Android.

Taarifa ya polisi iliyowasilishwa katika kituo cha polisi cha Kasarani inasema mshukiwa alikamatwa baada ya maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kufanya upekuzi katika nyumba yake siku ya Jumatatu.

 "Vitu hivyo vinashukiwa kuibiwa kutoka kwa umma," ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyofichuliwa kwa vyombo vya habari.

Polisi wanasema wamerekodi tukio hilo na mahojiano yanaendelea ili kubaini ni akina nani walioandamana na mshukiwa hao wakisubiri kufikishwa mahakamani Jumanne, Novemba 22.

Kukamatwa huko kunajiri siku chache baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuwaonya vijana wanaojihusisha na uhalifu.

“Wale vijana ambao wameithubutu serikali na kutaka kutuambia kuwa wanaweza kuuteka mji na kuufanya mji wa uhalifu, tumewasikia na kwa hiyo tunakuja mara moja,” alisema Kindiki katika onyo lake wiki moja iliyopita.

Katika muda wa wiki mbili ambazo zimepita, visa vya uhalifu na wizi wa kimabavu vimekuwa vikiripotiwa katika miji mbali mbali huku jiji kuu la Nairobi likiwa moja ya sehemu zilizoathirika pakubwa.

Kumekuwa na video mbali mbal iambazo zimekuwa zikisambazwa pamoja na picha zikionesha wahanga wa magenge hatari ya wezi ambao wanakuvamia na kukupokonya kila kitu kabla ya kukuacha na majeraha mabaya ili ujifie mwenyewe.

 Kufuatia hali ya usalama kuwa tete, rais William Ruto wiki jana aliunga mkono maafisa wa kulinda usalama kutumia silaha zao za bunduki kukabiliana na magenge hatari ya wezi katika kile alisema kuwa watu wa chini ni sharti walindwe kutokana na vijana hao ambao walitaka kuhatarisha usalama wa wakaazi wa Nairobi.

“Tumewapa silaha, sheria iko upande wenu, kuhakikisha kwamba mnakabiliana na majambazi kwa njia stahiki. Kama afisa yeyote ako hatarini ya majambazi, ni lazima atumie silaha yake kukabiliana na majambazi. Tusingoje maafisa wetu wakauawe na wakora, ni sharti tukabiliane na wakora kabla hawajakabiliana na maafisa wetu,” rais Ruto aliwaambia walinda usalama.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved