Nchini Kenya, utawasikia watu wanabananga msemo wa bahati kama ya mtende na kusema bahati kama ya Igathe, wengine utawasikia wanasema Mungu wa Igathe. Hivi huyu Igathe ni nani?
Basi habari za hivi punde zimedhihirisha kuwa aliyekuwa mgombea ugavana wa kaunti ya Nairobi kabla ya uchaguzi mkuu, Polycarp Igathe amejishindia nafasi ya kazi katika kampuni ya Tiger Brands.
Amepata kazi hiyo kama Mkurugenzi Mkuu wa Ukuaji wa kampuni kwenye kampuni hiyo ambayo iko Afrika Kusini.
Hapa awali, Igathe aliwahi kufanyia kampuni hiyo kazi kama Mkurugenzi Mtendaji wa Afrika Mashariki kabla ya kujiunga na kampuni ya Vivo Energy.
Tiger Brands ni kampuni kubwa kabisa ya vyakula nchini Afrika Kusini .
Polycarp Igathe ni jamaa msomi ambaye jina lake lilijinafasi katika ndimi za wengi baada ya ujio wake katika fani ya siasa za humu nchini.
Wengi wamekuwa wakimhusisha na bahati kutokana na dhana kwamba Igathe tangu maisha yake ya ujana mpaka sasa anaelekea hamsini, amekuwa ni mtu wa kutafutwa na kazi, na si yeye kutafuta kazi kama ilivyo kawaida kwa watu wengi.
"Wah!Nataka kufahamu hewa anayopumua Polycarp Igathe! Huyu ni mkuu wa miadi!" Janet Machuka alisema.
"Polycarp Igathe hutoa sadaka kila Jumapili, naenda kanisa moja naye, wewe hata sadaka hutaki kusikia na unataka kubarikiwa kama yeye," Kijana ya KU alisema.
"Igathe alisomea nini, niko tayari kurudi shule nisome alichosoma. Hii ni zaidi ya bahati. Yaani jamaa huyu anatoka kazi akiwa CEO, anaingia ya CFO, anatoka hio anakuwa COO huku mimi nikiwa sina kazi,"Richie alisema.
Baadhi ya kazi alizofanya Igathe ni kama:
- Afisa wa kifedha - Queensland Health, Australia.
- Mkufunzi wa usimamizi - CocaCola Africa.
- Meneja wa mauzo na masoko - Africa Online.
- Meneja wa uendeshaji wa mauzo - East Africa Breweries.
- Mkurugenzi Mtendaji - Haco
- Mkurugenzi Mtendaji - Vivo
- Mwenyekiti - Chama cha watengenezaji wa Kenya.
- Mwenyekiti - Taasisi ya Petroli Afrika Mashariki.
- Naibu Gavana - Nairobi.
- Afisa mkuu wa kibiashara - Equity Group Holdings.