Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amewahakikishia Wakenya kwamba mtihani wa kitaifa wa mwaka huu utakuwa wa kuaminika.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatau alipokuwa akisimamia usambazaji wa karatasi za mtihani wa KCPE na KPSEA, Machogu alisema kuwa serikali imeweka mikakati ya kiusalama kuhakikisha visa vya udanganyifu katika mitihani vinadhibitiwa.
Alisema karatasi za mitihani wa watahiniwa wa darasa la 8 na 6 zilifika kwa wakati katika vituo vyote 493 kote nchini.
Darasa la 6 lina zaidi ya watahiniwa milioni 1.6 waliosajiliwa kufanya mtihani wa KPSEA.
Siku ya Jumatatu, watahiniwa wa Darasa la 8 watafanya Hisabati, Kiingereza na Composition. Jumanne watakalia Sayansi, Kiswahili na Insha.
Na siku ya mwisho, watakuwa na karatasi za Mafunzo ya Jamii na Elimu ya Dini.
Wanafunzi wa darasa la 6 wataanza na Hisabati kama karatasi ya kwanza na Kiingereza siku ya Jumatatu.
Siku ya Jumanne, wanafunzi watatahiniwa katika Sayansi Jumuishi na Kiswahili.
Mtihani utakamilika Jumatano na Sanaa ya Ubunifu na Mafunzo ya Jamii.
Kwa Darasa la 6, masomo hayo yameunganishwa katika Sayansi Jumuishi tano ambazo ni Sayansi na Teknolojia, Kilimo, Sayansi ya Nyumbani, na Afya ya Kimwili.
Sanaa Ubunifu na Mafunzo ya Kijamii ni pamoja na masomo ya kijamii, elimu ya Kikristo, Kiislamu na Kihindu, sanaa na ufundi, na muziki.