Naibu Rais Rigathi Gachagua ameunga mkono matamshi ya Inspekta Jenerali wa polisi Japthet Koome kwamba maafisa wa polisi wanapaswa kutumia bunduki kujilinda.
Akizungumza katika kanisa moja katika Parokia ya Maralal Cathedral huko Samburu Jumapili, DP Gachagua alitoa maoni kwamba maafisa wa polisi wanapaswa kujilinda kila wanapotishwa na majambazi wanaotumia bunduki.
"Waziri wa Mambo ya Ndani na IG wa polisi wamezungumza na ningependa kusisitiza kwamba ili maafisa wa polisi wakulinde ni lazima wajilinde kwanza. Ikiwa una silaha, kutishia polisi haitakuwa nzuri," alisema DP Gachagua.
"Na hakuna ubaya. Kwa hiyo ukiwa na silaha usijaribu kuwatishia maafisa wa polisi. Ili askari polisi wakulinde ni lazima wajilinde, hivyo basi mtu yeyote asiwajaribu, itakuwa mbaya."
IG Koome, wakati wa ibada ya ukumbusho ya maafisa walioaga kutoka Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Huduma za Magereza ya Kenya katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi ya Utawala (APTC) mnamo Ijumaa, aliwahakikishia maafisa wa kuwaunga mkono iwapo watakamatwa kwa kujilinda na bunduki.