Wanafunzi watatu wa chuo kikuu cha Nairobi wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuzama kwa maji ya Mulokoba Waterfront katika kaunti ya Busia, eneobunge la Budalangi.
Watatu hao ambo walikuwa katika kikundi cha wanafunzi 7 wa chuo cha UON waliozuru kaunti ya Busia kujivinjari baada ya ziara ya huduma ya kusambaza injili walizama na boti yao Desemba 31 usiku.
Wanafunzi hao watatu, walikuwa katika Mwaka wa 6, Mwaka wa 3, na Mwaka wa Kwanza.
Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Bunyala Isaiah Mose alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa wengine wanne waliokolewa.
Miili ya watatu hao bado haijatolewa, kwa mujibu wa mkuu wa polisi, huku zoezi hilo likiahirishwa Jumamosi usiku baada ya giza kuingia. Msako huo, kulingana na OCPD wa Bunyala, unaendelea.
Kulingana na jarida la Star kisa hicho kinajiri siku chache tu baada ya kisa kingine cha ndugu wa toka nitoke Dedan Omondi Damai, 22, na Wycliffe Onyango Damai, 21, waliokuwa wameenda kuvua samaki katika ufuo huo kabla ya kukutana na kifo chao cha ghafla.
Inaarifiwa kuwa boti ambao wanafunzi hao walikuwa wanatumia ililemewa kufuatia mawimbi makali ambayo yalizuka wakati wameshafika ndani kabisa mbali kutoka ufukwe.
Shughuli ya kuitafuta miili yao ilisitishwa usiku wa Jumamosi kufuatia kiza kinene kuingia na ilitarajiwa kuendelea Jumapili tarehe mosi 2023.