Shirika la kiserikali linaloshughulikia masuala ya wanyama nchini India limetoa wito kwa raia wa taifa hilo kubusu ng’ombe siku ya wapendanao, Februari 14.
Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye majarida kutoka nchini humo, hatua hiyo ilitajwa kama moja ya kuendeleza utamaduni wa Kihindi, kuonesha mapenzi kwa wanyama haswa ng’ombe.
Bodi ya Ustawi wa Wanyama ya India ilisema Jumatano kwamba "kukumbatia ng'ombe kutaleta utajiri wa kihisia na kuongeza furaha ya mtu binafsi na ya pamoja."
Wahindu wacha Mungu, wanaoabudu ng'ombe kuwa watakatifu, wanasema sikukuu hiyo ya Magharibi inapingana na maadili ya kitamaduni ya Wahindi.
Jarida la Washington Post liliripoti kuwa katika miaka ya nyuma, Wahindi wenye itikadi kali kwa utamaduni wao wamekuwa wakishambulia maduka na kuvunja maua wakati wa siku ya Februari 14 wakisema kuwa siku hiyo ya wapendanao ni ya Wazungu kutoka nchi za magharibi na nia yao ni kupigia debe usherati.
Baadhi ya watu sasa wanahisi hatua ya serikali kuwataka watu kubusu ng’ombe ni nzuri kwani inakuja kuvunja miiko na tamaduni hizo za kutotaka watu kusherehekea wapendwa wao katika taifa hilo lenye idadi ya watu wengi duniani.
“Serikali ya Kihindu inayoongozwa na Waziri Mkuu Narendra Modi imekuwa ikisukuma ajenda ya Kihindu, kutafuta ukuu wa dini hiyo kwa gharama ya taifa lisilo la kidini linalojulikana kwa utofauti wake. Wahindu wanajumuisha karibu 80% ya watu wake karibu bilioni 1.4. Waislamu ni asilimia 14, huku Wakristo, Masingasinga, Mabudha na Majaini wakichukua sehemu kubwa ya 6% iliyobaki,” jarida moja liliripoti.
Ng'ombe, kwa muda mrefu nchini humo amekuwa akionwa kama mnyama mtakatifu miongoni wa Wahindi na anaheshimiwa sana na wengi sawa na mama ya mtu. Majimbo mengi nchini India yamepiga marufuku kuchinja ng'ombe. Ombi la bodi ya ustawi wa wanyama linawataka watu watoke nje na kuwakumbatia ng'ombe mnamo Februari 14.