Mwenyekiti wa chama cha KANU ambaye pia alikuwa seneta wa Baringo Gideon Moi amewasherehekea wanawake tajika waliofanya mambo makubwa ya kupigiwa mfano siku huu ya kimataifa ya wanawake.
Moi alisema kwamba kuna mengi mazuri ambayo wakenya wanaweza kuwakumbuka wanawake na kuwasherehekea nayo.
“Kuna mengi ya kusherehekea kuhusu wanawake katika Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake na kila siku nyingine; mafanikio yao, uthabiti na ukweli tu kwamba wao ni wanawake. Na wanawake watatu wachanga wanakuja akilini,” Moi alianza.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Moi alimsherehekea Nelly Cheboi, mwanamke aliyetuzwa kama shujaa na runinga ya CNN mwishoni mwa mwaka jana kwa juhudi zake za kueneza dijitali katika vijiji vya Kenya.
“Tunampigia saluti Nelly Cheboi - mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa TechLit Africa - kwa kutawazwa kwake kama shujaa wa Mwaka wa CNN 2023. Kwa kutoa ufikiaji wa kompyuta kwa shule za vijijini na kutoa ujuzi wa kiteknolojia miongoni mwa wanafunzi, amechangia kwa kiasi kikubwa katika kuziba mgawanyiko wa kidijitali katika mfumo wetu wa elimu,” Moi alianza.
Kando na Cheboi, Moi pia aliwasherehekea wanawake wengine kama nesi maarufu kutoka Marsabit Anna Duba, mchezaji mchanga katika mchezo wa tenisi Angela Okutoyi miongoni mwa watu wengine ambao aliwataja kama vielelezo bora kwa wanawake wote nchini ambao wanafaa kusherehekewa.
“Bila shaka, Anna Qabale Duba alipanda kutoka kijiji kisichojulikana sana katika Kaunti ya Marsabit hadi kiwango cha kimataifa baada ya kutunukiwa kuwa Muuguzi Bora Duniani. Katika uwanja wa michezo, Angella Okutoyi ni gwiji wa tenisi. Aliibuka mshindi wa mechi ya Wasichana Singles Grand Slam wakati wa Australian Open 2022, na kuwa Mkenya wa kwanza kufuzu hadi raundi ya tatu ya Grand Slam. Hili si jambo la mzaha,” Moi alisema.
Kwa kweli, wanawake ni wa ajabu. Heri ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.