Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma mnamo Alhamisi, Machi 9, ilikanusha ripoti zinazodai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alikuwa amepokea ripoti ya kesi ya ardhi inayomkabili aliyekuwa makamu wa rais, Kalonzo Musyoka.
Katika taarifa, ODPP ilionyesha kuwa ripoti hizo ni ghushi na za kupotosha. Pia aliwataka wananchi kupuuza habari hiyo inaodaiwa kuwa imetoka ofisini kwake.
"ODPP ingependa kufahamisha umma kwamba taarifa kwenye bango lililoambatishwa ni ya kupotosha na si ya kweli," ilisoma taarifa hiyo.
Chapisho lililoenea kwenye mitandao ya kijamii likiwa na picha ya DPP Haji lilidai kuwa Kalonzo alikuwa anachunguzwa.
Kulingana na ripoti hizo bandia, DPP Haji alidai kuwa uchunguzi ulihitimishwa, na alikuwa akipokea ripoti ya mwisho.
“Nimepokea ripoti inayoelezea matokeo ya uchunguzi wa madai ya unyakuzi wa ardhi ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na aliyekuwa Makamu wa Rais Mhe. Kalonzo Musyoka. Nitapitia faili na kushauri kuhusu hatua zinazofaa,” ilidai taarifa hiyo.
Hapo awali, Makamu wa Rais wa zamani alitupilia mbali madai kama hayo, akisema kwamba wapinzani wake walieneza kwa manufaa ya kisiasa.
Akihutubia madai hayo mwaka wa 2021, Kiongozi wa Chama cha Wiper alitoa wito kwa mashirika ya uchunguzi kuchunguza na kusuluhisha suala hilo la mara kwa mara kwenye sehemu ya ardhi.
Kalonzo alijiwasilisha kwa hiari yake mbele ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili kuhojiwa ili kufuta jina lake kutokana na madai yanayohusu uwezekano wa mchakato usiofuata utaratibu wa kupata kipande cha ardhi huko Yatta kaunti ya Mahakos.