logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Utata huku kijana mwingine akifariki baada ya kudaiwa kuanguka kutoka paa ya ghorofa Kasarani

Blair Muthomi ,23, alipatikana amefariki nje ya nyumba aliyokuwa akiishi katika eneo la Mwiki, Kasarani.

image
na Samuel Maina

Habari12 March 2023 - 08:30

Muhtasari


  • •Mwili wa Muthomi ulipatikana ukiwa amelala sakafuni baada ya kudaiwa kuanguka kutoka juu ya paa nyumba hiyo.
  • •Mamake marehemu alitaka  uchunguzi wa kina huku akidokeza kwamba kunaweza kuwa na mchezo mchafu.

Wapelelezi wameanzisha uchunguzi baada ya kijana wa miaka 23 kupatikana amefariki nje ya nyumba aliyokuwa akiishi katika eneo la Mwiki, Kasarani.

Mwili wa Blair Muthomi  ulipatikana ukiwa amelala sakafuni siku ya Ijumaa baada ya kudaiwa kuanguka kutoka juu ya paa nyumba hiyo ya ghorofa.

Marehemu anaripotiwa kuanguka na kichwa kwanza ndani ya shimo lililo katika eneo la ujenzi lililo karibu na ghorofa hiyo. Alikuwa akiishi na marafiki zake wawili na alikuwa akingoja kuhitimu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Nairobi hivi karibuni baada ya kumaliza masomo yake ya Uhandisi wa Mitambo.

Mwili wa Muthomi ulionekana na mwenye nyumba, Bw Joseph Macharia, ambaye alifahamisha wenzake wawili mara moja na wakamkimbiza hospitalini wakidai kuwa bado alikuwa akipumua. Hata hivyo, alitangazwa kuwa amefariki punde baada ya kufikishwa hospitalini na wazazi wake wakafahamishwa.

Familia ya marehemu ambayo ilishtushwa sana na kifo chake cha kutisha ilipata ugumu wa kuelewa kilichotokea. Walisema kuwa viungo vyake vya mwili vilikuwa vimeharibiwa vibaya, ishara kuwa  kilikuwa kifo cha uchungu sana.

Mamake Muthomi, Kajuju Mwiathi alimtaja mwanawe kama kijana mzuri aliyekuwa wa msaada mkubwa kwa familia.

"Naskia nikiwa na moyo mgumu sana kwa sababu huyo ni kijana wangu wa kwanza. Hata hatujawafahamisha ndugu zake. Sijui cha kuwaambia. Amekuwa kama baba kwa hao watoto," Bi Mwiathi alisema.

Alitoa wito wa uchunguzi wa kina katika kifo cha mwanawe wa kwanza huku akidokeza kwamba kunaweza kuwa na mchezo mchafu.

"Ningetaka haki itendeke kwa huyu mtoto, angalau tujue sababu ya kifo chake," alisema

Polisi tayari wamewazuia wenzake wawili na watasaidia katika uchunguzi. Uchunguzi wa maiti pia umefanywa kwenye mwili wake.

Wanapatholojia walisema Muthomi alifariki kutokana na majeraha ya tumbo na kifua ambayo yalisababishwa na kuanguka. Polisi hata hivyo bado wanachunguza iwapo kulikuwa na mchezo mchafu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved