Wachezaji wawili wa kandanda wauawa kwa kupigwa na radi Kisii

Wengine wawili wanauguza majeraha katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira ambapo walikimbizwa kwa matibabu.

Muhtasari

•Timu hizo - Manyansi na Nyagiti- zilikuwa zikicheza mechi ya kirafiki wakati wa tukio hilo la saa kumi unusu alasiri.

•Mchezaji mmoja alifariki katika eneo la tukio huku wa pili akifariki akiwa hospitalini ambako alikimbizwa kwa matibabu ya dharura.

Rip
Rip
Image: HISANI

Wasimamizi wa kandanda katika eneo la Kitutu Chache, Kisii, wanasema kuwa wachezaji wawili wa kandanda waliuawa na radi wakati wa mechi iliyokuwa ikiendelea kwenye uwanja wa Manyansi.

Timu hizo - Manyansi na Nyagiti- zilikuwa zikicheza mechi ya kirafiki wakati wa tukio hilo la saa kumi unusu alasiri.

Waliofariki walitambuliwa kuwa ni Sammy Musa, 20, na Joshua Nyangaresi, 21.

OCPD wa Marani, Benlife Munuve, alisema mchezaji mmoja alifariki katika eneo la tukio huku wa pili akifariki akiwa hospitalini ambako alikimbizwa kwa matibabu ya dharura.

Evans Akanga, Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kaskazini la Kitutu Chache, alisema wachezaji hao walifariki Jumamosi jioni wakati wa mchuano wa kirafiki.

Wachezaji wengine wawili wanauguza majeraha katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira ambapo walikimbizwa kwa matibabu.

"Timu zilikuwa na mechi ya kirafiki wakati mvua ilianza kunyesha ghafla," alisema.