Makundi ya waandamanaji, haswa wafuasi wa Azimio-One Kenya yalianza kumiminika nje ya jumba la KICC siku ya Jumatatu asubuhi kabla ya maandamano yaliyotangazwa na kiongozi wa muungano huo, Raila Odinga kung'oa nanga.
Huku baadhi yao wakiwa wamejihami kwa sufuria, vijiko, sahani na vitu vingine, waandamanaji hao waliimba na kucheza densi huku wakisubiri viongozi wao kuwasili ili maandamano yaanze rasmi.
Baadhi ya waandamanaji walisikika wakiimba "Ruto must go!" Kumaanisha (Ni lazima Ruto aende!)
Wengine waliimba "Unga! Unga! Unga!" huku wakijumuika pamoja.
Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna aliwahutubia waandamanaji hao na kuwapa ratiba ya siku.
"Kutoka hapa tunaelekea Ikulu. Kila mtu sasa akuje KICC tumefungua milango ya KICC," Sifuna alisema.