Mamlaka ya mawasiliano nchini CA imetoa orodha ya vituo vya runinga 6 ambavyo vilienda kinyume na maadili ya upeperushaji wa matukio katika kuonesha matukio ya maandamano mapema Jumatatu Machi 20.
CA walisema kwamba tayari imeziandikia barua runinga hizo ikizitaka kuchukua hatua mwafaka.
Katika barua hiyo, CA ilisema kwamba matukio ambayo yalipeperushwa na runigna hizo 6 yalikwenda kinyume na maadili ya kupeperusha kwani yalilenga kuzua taharuki na uwiano miongoni mwa Wakenya, hivyo kuliweka taifa katika mkondo mbaya wa kuvuruga Amani.
“Vituo sita vya Televisheni, NTV, Citizen TV, K24T, KBC, TV47, na Ebru Tv vilikiuka Kanuni za Utayarishaji wa vipindi wakati wa kutangaza maandamano ya upinzani Jumatatu. Utangazaji wa vituo hivyo ulionyesha matukio ambayo yanaweza kusababisha hofu au uchochezi kwa umma, na kutishia amani na mshikamano nchini. Kwa mujibu wa sheria, CA imeziandikia vyombo sita vya habari kuchukua hatua za kurekebisha,” Sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.
“Wakati Mamlaka inakuza uhuru wa vyombo vya habari, ni muhimu kwamba watangazaji wote wawe waangalifu katika utangazaji wa moja kwa moja ili kuepuka matukio ambayo yanaweza kuhatarisha amani na mshikamano,'' alisema Mkurugenzi Mkuu wa CA Ezra Chiloba.
Muungano wa upinzani Jumatatu uliandaa maandamano katika baadhi ya miji nchini haswa jijini Nairobi ambapo Odinga aliwataka wafuasi wake kujumuika ili kuanza maandamano kwenda ikulu kuwasilisha ujumbe wao kwa rais.
Katika upeperushaji huo wa moja kwa moja ambao CA imetangaza kama ulikwenda kinyume, runinga nyingi zilionesha jinsi watu walikuwa wanakabiliana na maafisa wa polisi kwa kuwatupia mawe huku polisi wakijibu kwa kuwatupia vitoa machozi na maji.