Mjasiriamali na mrithi wa kampuni ya vileo ya Keroche Anerlisa Muigai ameibuka na jipya kuhusu kigezo cha kutathmini wanaume kamili na wanaume magumegume.
Kwa mujibu wa mfanyibiashara huyo, mwanamume kamili ambaye ana utimamu wa kufurahia maisha kwa kujizolea utajiri na afya nzuri na kukimu familia vizuri, mwanamume huyo hafai kujipata au kupatikana katika mitandao ya kijamii hata kidogo.
Muigai anahisi kwamba mwanamume ambaye ako katika mitandao ya kijamii haswa haswa Instagram, TikTok na Snapchat, huyo si mwanamume wa kutegemewa kuwa atakuza familia au hata kujikuza mwenyewe.
Muigai alisema kwamba mwanamume kamili kama itabidi yeye kupatikana mitandaoni basi huwa ni mchache sana kwani muda mwingi hayuko kule bali anajishughulisha na masuala ya kumletea tija maishani.
“Mwanamume kamili hawezi kuwa na Instagram, Snapchat na TikTok kwa wakati mmoja. Wanaume kamili wa ukweli kabisa huwa hawapatikani kwenye mitandao ya kijamii. Na kama wanapatikana huko, basi huwa hawaitumii mitandao hiyo muda wote, angalau asilimia kubwa yao,” Muigai alisema.
Hii si mara ya kwanza kwa mrithi huyo wa Keroche kuibua vigezo vya kuwatambua wanaume kamili.
Wiki jana, Muigai kupitia instastory yake aliibua kigezo kingine akiashiria kwamba hakuna mwanamke anayepata furaha ubavuni mwa mwanamume maskini.
Muigai alipakia video iliyomuonesha mwanamume akiigiza kama mfumo wa kutoa pesa wa ATM huku mwanamke akimbofya kifuani kabla ya mwanamume huyo kuchomoza bunda la noti na kumkabidhi mwanamke aliyeng’aa kwa tabasamu pana usoni.
Muigai alisema furaha ya kila mwanamke ni mwanamume mwenye pesa, na kuwataka wanaume waache kujilaza kizembe na badala yake kutafuta hela kwa namna zote.