Kwa mara nyingine tena, wakaazi wa Ndarugo, katika barabara kuu ya Thika walijikuta katika hekaheka za hapa na pale kujizolea chakula baada ya gari lililokuwa likisafirisha avocado kuanguka sehemu hiyo.
Katika picha ambazo zilisambazwa mitandaoni Alhamisi, makumi ya watu walionekana waking’ang’ana kujizolea avocado hizo ambazo zilikuwa zimetapakaa barabarani baada ya ajali.
Hii inatokea siku tano tu baada ya lori lililokuwa likisafirisha shehena ya mahindi na maharagwe pia kupata ajali sehemu hiyo hiyo na mamia ya watu kufurika wakijizolea chakula hicho.
Usafiri katika barabara ya Thika, Jumamosi, Machi 25, ulitatizika baada ya lori hilo lililokuwa likisafirisha mahindi na maharagwe kupinduka kwenye barabara kuu yenye shughuli nyingi.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa lori hilo lilipinduka kuzunguka Ndarugo - karibu na Juja, dakika chache baada ya saa 10 alfajiri.
Madereva wanaotumia barabara hiyo walirekodiwa wakipora mahindi na maharagwe kwenye mifuko ya guinea, kwani wengi wao waliweka mazao ya shambani kwenye magari yao kabla ya kuondoka.
Lori lililopinduka liliziba njia ya magari yaliyokuwa yakielekea Wilaya ya Biashara ya Nairobi (CBD).
Eneo la Ndarugo sasa limegeuka kuwa gumzo mitandaoni, baadhi wakizua utani kwamba Mungu anapenda watu wa eneo hilo kwani amekuwa akiwaletea vyakula kwa njia ya bwerere pasi na kutarajia, wakati huu ambapo maandanamo yanaendelea kote nchini kulalamikia gharama ya juu ya maisha na ugumu wa maisha.