Kasisi Paul Mackenzie ambaye amegonga vichwa vya habari kwa muda sasa kwa ajali ya dhehebu potovu ambayo yameshuhudia makumi ya watu kuaga dunia amewaonya Wakenya dhidi ya kujiingiza katika shughuli za kanisa lake.
Katika video iliyoonekana na gazeti la Star, Mackenzie alitoa onyo hilo akiwa kwenye gari la polisi muda mfupi baada ya kukamatwa Aprili 15.
Anasikika kwenye video hiyo akiwaonya polisi na watu waliokuwa wamekusanyika karibu na gari la polisi kutoliangalia suala hilo kwa sababu litakuja kuwaandama.
"Mnachopigana nacho hamkijui na kitawaramba, kitawaramba nawaambia."
Mackenzie anashukiwa kuwafunza wafuasi wa Kanisa lake la Good News International katika kufunga hadi kufa kwa imani ya kupaa mbinguni.
Kufikia Jumanne adhuhuri, wapelelezi walikuwa wamefukua miili 90 katika kipande chake cha ardhi cha ekari 800 katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.
Miili hiyo ilitolewa kwenye makaburi yenye kina kifupi ambapo inaaminika kuzikwa baada ya kifo chao.
Watu 32 hadi sasa wameokolewa wakiwa hai kwenye kaburi hilo la kutisha la umati.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alizuru eneo hilo na kutaja vifo hivyo kuwa ni mauaji ya halaiki. Alitangaza eneo hilo kuwa eneo la uhalifu.