logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Dhebehu la Shakahola: Watoto ndio waliolengwa kufa kwanza - mhubiri msaidizi wa zamani

Kufikia sasa polisi wamefukua miili 201 katika msitu ulioko kusini mashariki mwa Kenya.

image
na SAMUEL MAINA

Habari15 May 2023 - 03:52

Muhtasari


  • •Mhubiri msaidizi wa zamani wa ibada hiyo aliliambia gazeti la New York Times kwamba watoto waliuawa kwanza, na kuamriwa "kufunga kwenye jua ili wafe haraka."
  • •Uchunguzi rasmi wa baadhi ya miili katika shamba kubwa la Shakahola, karibu na mji wa pwani wa Malindi, ulibaini dalili za njaa, kukosa hewa na kupigwa.

Watoto walikuwa wakilengwa kuwa wa kwanza kufa kwa njaa katika siku za mwisho za ibada ya siku ya maangamizi iliyoendeshwa na kanisa moja dhehebu la kikiristo linaloamini kufunga hadi kufariki dunia huko nchini Kenya, kulingana na ushahidi mpya unaoibuka.

Polisi wanaochunguza kesi inayoonekana kuwa kujitoa mhanga hadi sasa wamefukua miili 201 katika msitu ulioko kusini mashariki mwa Kenya.

Mhubiri msaidizi wa zamani wa ibada hiyo aliliambia gazeti la New York Times kwamba watoto waliuawa kwanza, na kuamriwa "kufunga kwenye jua ili wafe haraka."

Wanawake na wanaume walikuwa wakifuatia kwa utaratibu huo katika mpango wa kujiua, Titus Katana alisema.

Bw Katana - ambaye anawasaidia polisi katika uchunguzi - pia alielezea kwa Sunday Times madai ya kutendewa ukatili watoto hao, akisema walifungiwa kwenye vibanda kwa siku tano bila chakula wala maji.

“Kisha wakawafunga blanketi na kuwazika, hata wale ambao bado wanapumua,” alinukuliwa akisema.

Inadaiwa kuwa wafuasi wa dhehebu hilo waliambiwa wangefika mbinguni haraka ikiwa wangekufa kwa njaa.

Uchunguzi rasmi wa baadhi ya miili katika shamba kubwa la Shakahola, karibu na mji wa pwani wa Malindi, ulibaini dalili za njaa, kukosa hewa na kupigwa.

Zaidi ya watu 600 wanaoripotiwa kuwa washiriki wa ibada ya siku ya maangamizi inayodaiwa kuongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie bado hawajulikani walipo.

Mchungaji Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi, alisema alifunga Kanisa lake la Good News International miaka minne iliyopita baada ya takriban miongo miwili ya operesheni.

Lakini BBC ilikuwa imefichua mamia ya mahubiri yake ambayo bado yanapatikana mtandaoni, ambayo baadhi yake yalionekana yalirekodiwa baada ya tarehe hii.

Katika mahojiano na gazeti la Daily Nation la Kenya wiki chache zilizopita, Mchungaji Mackenzie pia alikanusha kuwa aliwalazimisha wafuasi wake kujilaza kwa njaa.

Lakini Mchungaji Mackenzie alihubiri dhidi ya elimu, akisema kwamba ilikuwa ya kishetani, baada ya kupokea "ufunuo kutoka kwa Mungu", Bw Katana aliambia New York Times.

Akieleza sababu zake za kuacha dhehebu hilo, Bw Katana, ambaye pia anasaidia katika uchunguzi wa polisi dhidi ya mchungaji huyo, alisema mafundisho yake yamekuwa ya "ajabu sana".

Mchungaji Mackenzie pia aliwahimiza akina mama kuepuka kutafuta matibabu wakati wa kujifungua na kutowachanja watoto wao.

Mengi ya mahubiri ya Mchungaji Mackenzie yanahusiana na utimizo wa unabii wa Biblia kuhusu Siku ya Hukumu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved