Mama akamatwa baada ya kurekodiwa akimlazimisha mwanawe wa kambo kula kinyesi chake

Mtoto huyo kwa sasa yuko kwenye makazi salama ambapo anatunzwa.

Muhtasari

•Video ya Esther Nabirie akimfanyia mtoto huyo kitendo hicho kiovu ilisambaa mitandaoni siku chache zilizopita na kuzua hasira miongoni mwa wanamitandao,  hali iliyosababisha polisi kuchukua hatua.

Mshukiwa akiwa ametiwa pingu ndani ya seli.
Mshukiwa akiwa ametiwa pingu ndani ya seli.
Image: HISANI

Mwanamke wa Uganda mwenye umri wa miaka 26 ambaye alirekodiwa kwenye kamera akimlazimisha mtoto wake wa kambo wa miaka minne kula kinyesi kwa sasa yuko kizuizini baada ya kukamatwa siku ya Jumatatu, Mei 16.

Video ya Esther Nabirie akimfanyia mtoto huyo kitendo hicho kiovu ilisambaa mitandaoni siku chache zilizopita na kuzua hasira miongoni mwa wanamitandao,  hali iliyosababisha polisi kuchukua hatua.

Akithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa, msemaji wa polisi Fred Enanga alisema kuwa mwanamke huyo atafikishwa mahakamani ambapo atakabiliwa na mashtaka ya kutesa watoto. Pia aliwapongeza majirani wa Nabirie kwa kurekodi tukio hilo na kusaidia kukamatwa.

“Tumefanikiwa kumkamata Esther Nabirie, mke wa Mugavis mwenye umri wa miaka 26 ambaye ni fundi mitambo baada ya kunaswa kwenye video akimlazimisha mtoto mdogo wa miaka 4 na nusu kula kinyesi chake. Yuko chini ya ulinzi wetu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Jinja na tumefungua kesi ya kuteswa na kunyanyaswa kwa mtoto dhidi ya Nabirie. Tunataka kuwashukuru majirani kwa sababu tuliweza kuingia kwa kasi sana, hilo lilikuwa tendo la ujasiri,” Enanga alisema.

Msemaji huyo wa polisi alidokeza kuwa mshukiwa huyo anaweza kukabiliwa na mashtaka zaidi kwani wanashuku kuwa angeweza kumsababishia mtoto huyo ukatili wa hali ya juu, jambo ambalo bado wanachunguza.

Mtoto huyo kwa sasa yuko kwenye makazi salama ambapo anatunzwa.