Kaimu kiongozi wa chama cha Jubilee Sabina Chege amesema kuwa aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliondolewa kihalali kama kiongozi wa chama hicho.
Kuna makundi mawili ya chama cha Jubilee, moja likiongozwa na Mbunge wa EALA, Kanini Kega na lingine la aliyekuwa Mbunge wa Ndaragwa, Jeremiah Kioni, ambao wote wanadai kuwa viongozi waaminifu wa chama hicho.
Akizungumza katika ibada ya mazishi katika eneo bunge la Sirisia siku ya Jumamosi, Chege alimshutumu Rais wa zamani kwa kujihusisha kikamilifu na siasa badala ya kutoa mwongozo kwa viongozi walio afisini.
Alibainisha kuwa marais wa zamani wanapaswa kustaafu kutoka kwa siasa miezi sita baada ya marais wapya kuchukua madaraka.
"Hakuna aliyemfukuza Uhuru Kenyatta kuwa mkuu wa chama cha Jubilee, tulifuata sheria kumwondoa," alisema.
Kaimu katibu mkuu Kanini Kega kwa upande mwingine, alimshutumu Uhuru kwa kutumia wadhifa wake kuwahangaisha wengine. Alisema kesi ya mbunge wa Sirisia John Waluke ilikuwa ya kisiasa.
"Kusema kweli mateso ya Waluke yalikuwa ya kisiasa, Uhuru Kenyatta alitumia nafasi yake kuwanyanyasa wengine," Kega alisema.
Aidha, kaimu viongozi wa chama hicho walimtaka Rais huyo wa zamani kuzingatia kuwaunganisha Wakenya kama anavyofanya katika mataifa mengine ya Afrika.
"Baada ya Uhuru kustaafu, alipewa jukumu la kuhakikisha kuwa kuna amani barani Afrika lakini jinsi anavyotenda inaonekana hafanyi kile kinachohitajika," Chege aliongeza.
Chege alibainisha kuwa wakiwa chama cha Jubilee, wanaunga mkono kikamilifu serikali ya Rais William Ruto.
"Kama chama cha Jubilee, hatutashiriki maandamano yanayoongozwa na mkuu wa chama cha ODM, ni kupoteza muda," alisema.
Aliongeza kuwa Uhuru alimpa kwa hiari zana za mamlaka Rais Ruto. Aliomba upande pinzani umpe muda wa kuwafanyia kazi Wakenya.
"Kuna walaghai Nairobi wanaojifanya kuwa maafisa wa dhati wa Jubilee, hatuwajui, hao ni wafuasi wa ODM wanaojaribu kuleta mkanganyiko katika chama chetu," alisema.