Bandari ya Dar, yaipiku Mombasa katika orodha mpya ya Benki ya Dunia

Muhtasari

•Bandari za Dar es Salaam, Djibouti na Berbera zimeipita Mombasa katika orodha ya hivi punde ya Benki ya Dunia kwenye bandari zenye ufanisi zaidi.

•Bandari kuu ya Kenya ilirekodi kushuka kwa kasi kutoka kwa ripoti ya 2021 ambapo iliwekwa katika nafasi ya 296 na Benki ya Dunia.

Image: BBC

Bandari za Dar es Salaam, Djibouti na Berbera zimeipita Mombasa katika orodha ya hivi punde ya Benki ya Dunia kwenye bandari zenye ufanisi zaidi, ikionyesha hofu ya ushindani ambayo Kenya imekuwa nayo juu ya Tanzania kuwa njia inayopendelewa kwa wasafirishaji.

Toleo la tatu la Matokeo ya Utendaji kazi wa Bandari ya Kontena duniani limeweka bandari ya Mombasa katika nafasi ya 326 mwaka wa 2022 kati ya bandari 348 duniani kote ambazo zilitathminiwa, nyuma ya bandari hizo za Afrika mashariki.

Bandari kuu ya Kenya ilirekodi kushuka kwa kasi kutoka kwa ripoti ya 2021 ambapo iliwekwa katika nafasi ya 296 na Benki ya Dunia.

Bandari hizo zimeorodheshwa kulingana na ufanisi wao, unaopimwa na muda uliopita kati ya wakati meli inafika bandarini hadi kuondoka kutoka kwenye kituo ikiwa imekamilisha kubadilishana mizigo.

Benki ya Dunia inabainisha kuwa uendeshaji mzuri wa bandari hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya biashara katika eneo hilo, ikisema kuwa kumekuwa na uboreshaji mkubwa katika biashara tangu 2020 wakati sekta ya usafiri wa baharini ilirekodi shughuli zilizopunguzwa kutokana na janga la Covid-19.

"Kuboresha ufanisi wa bandari ni muhimu kwa kufungua ukuaji na maendeleo ya Afrika," alisema Martin Humphreys, mwanauchumi mkuu wa usafiri katika Benki ya Dunia.

"Bandari za Afrika ni lango muhimu kwa biashara na uendeshaji bora unachangia usalama wa chakula. Uendeshaji wao wenye ufanisi ni kigezo muhimu cha kuamua ikiwa Afrika itafikia uwezo wake wa kiuchumi."

Haya yanajiri wakati Bandari ya Dar es Salaam ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imekuwa na ushindani mkubwa, na kutishia kuvuta meli nyingi zinazoingia katika bahari ya Afrika Mashariki kwenye bandari yao.

Katika orodha hiyo, bandari ya Tanzania ilirekodi kuimarika kutoka nafasi ya 2021 hadi kushika nafasi ya 312 kutoka 361 ya awali.

Takwimu kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) zinaonyesha kiasi cha mizigo inayohudumiwa na bandari ya Mombasa kilishuka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano mwaka wa 2022, huku wadau wakiashiria kuongezeka kwa ushindani kutoka Dar es Salaam.

Jumla ya shehena ya mizigo bandarini ilipungua hadi tani milioni 33.74 mwaka jana kutoka tani milioni 34.76 mwaka uliopita, kulingana na KNBS.

Kushuka kwa asilimia 2.93 kwa mwaka kulifanya idadi hiyo kuwa ya chini kabisa tangu 2018 ilipofikia tani milioni 30.92.