Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amemkashifu Rais William Ruto kuhusu nia yake katika chama cha Jubilee.
Akizungumza Jumatatu, Uhuru alitilia shaka nia ya Ruto ikiwa anaamini kuwa chama hicho kimekufa.
Mkuu huyo wa zamani wa nchi aliwaambia wajumbe kwamba chama bado kiko imara na kiko hai, hivyo basi maslahi kutoka kwa utawala wa Kenya Kwanza.
"Mnasema kwamba chama chetu imekufa, nani ana haja na maiti jamani? Kama imekufa why are you interested? Ukiona wanaitafuta jua haijakufa. We are very much alive na wataiona,"Alisema.
Uhuru alikuwa akijibu majaribio ya chama tawala kutaka viongozi waliochaguliwa wa Jubilee waunge mkono serikali.
Wabunge wanaomuunga mkono Ruto wakiongozwa na mbunge wa EALA Kanini Kega wameunda mrengo wao ndani ya chama na hawamtambui Uhuru kama kiongozi wa chama.
Uhuru wakati wa hotuba yake alitoa wito kwa wale wanaohisi kutoridhika kuwa ndani ya Jubilee kukihama chama hicho na kwenda popote wanapotaka.
Alimkashifu Rais William Ruto kuhusu jaribio la hivi majuzi la 'kuteka nyara' chama cha Jubilee.
Uhuru alisema kuwa hatatikiswa na kutikiswa na vitisho.
"Kuna wale ambao wanadhani kazi yao ni ya vitisho. Lakini sasa wajaribu mwingie , sio mimi,walijaribu kuiba kondoo na kuchoma kichaka wakifikiria tutaogopa lakini waendelee, pia ni haki yao kutoa matusi."
Uhuru amesema alifika katika afisi za Jubilee kutetea mali ya chama.
"Siku hiyo, sikujua ni kwa nini walivamia afisi ya Jubilee, niliposikia kuwa walienda huko, niliamua kwamba nitaenda ofisini na kutetea mali yetu hata nikiwa peke yangu," amesema.
"Ninasikia watu wakizungumza kwamba waliniona nikitembea na wavulana wadogo, lakini nataka kuwashukuru vijana wa kiume waliokuja kutetea chama chao. Niliwakuta huko na wengi wao si wa Jubilee lakini walikuwepo kwa ajili ya haki."
Haya yanajiri baada ya Uhuru kufika katika makao makuu ya Jubilee Kileleshwa mnamo Aprili 26.