Mwanamke mmoja wa Ecuador amefariki siku chache baada ya waombolezaji waliokuwa kwenye mazishi yake kushtuka kumpata akiwa hai ndani ya jeneza lake.
Bella Montoya, 76, alitangazwa kuwa amefariki kwa mara ya kwanza na daktari katika hospitali moja katika mji wa Babahoyo wiki iliyopita.
Lakini waombolezaji waliohudhuria mkesha wake waliposikia akigonga jeneza lake, mara moja alirejeshwa katika hospitali hiyo hiyo kwa matibabu.
Baada ya siku saba katika uangalizi maalum, wizara ya afya ya Ecuador ilithibitisha kuwa alikufa siku ya Ijumaa kutokana na kiharusi.
Taarifa ya wizara hiyo iliongeza kuwa amebakia chini ya "uangalizi wa kudumu" akiwa hospitalini.
Kufuatia kifo chake tarehe 16 Juni, Bi Montoya alirejeshwa katika nyumba moja ya mazishi kabla ya kuzikwa kwenye makaburi ya umma, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.
Tume ya wataalam imekusanywa na wizara ya afya ya Ecuador ili kukagua kesi yake.
Bi Montoya aliwekwa kwenye jeneza na kupelekwa kwenye chumba cha mazishi huko Babahoyo, kusini-magharibi mwa mji mkuu Quito, baada ya kutangazwa kuwa amefariki tarehe 9 Juni.
Lakini baada ya karibu saa tano ndani, mwanamke huyo alishtuka baada ya jamaa zake kufungua jeneza kubadilisha nguo zake kwa ajili ya mazishi.
Dakika chache baadaye, alitolewa nje na wazima moto na kurudishwa katika hospitali hiyo hiyo.
Bella Montoya sio mtu pekee "kuwa hai" baada ya kutangazwa rasmi kuwa amefariki.
Mnamo Februari, mwanamke mwenye umri wa miaka 82 alipatikana akipumua akiwa amelala katika nyumba ya mazishi katika Jimbo la New York.Alikuwa ametangazwa kuwa amefariki saa tatu mapema katika makao ya wazee.