Mchungaji mwenye utata kutoka mkoa wa Mwanza kaskazini mwa taifa jirani la Tanzania, Mfalme Zumaridi anaripotiwa tena kujipata kwenye ugomvi na vyombo vya dola kwa mara nyingine kutokana na video ambayo imeenezwa ikimuonesha akiwahubiria watoto kuwa hakuna Mungu mwingine isipokuwa yeye.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka taifa hilo Kusini mwa Kenya, Mfalme Zumaridi ambaye mwaka jana alijikuta nyuma ya nondo kwa tuhuma kama hizo alionekana tena akirudia kosa lilo hilo ambapo anaonekana akijitutumua pakubwa mbele ya makumi ya watoto, akiwaambia kuwa Mungu ni yeye tu wala hakuna na hakutatokea Mungu mwingine.
"Zumaridi ndiye Mungu wako na ndiye msaada wako, Zumaridi ndiye anakutenga na mauti, Mfalme Zumaridi ni Mungu wako chini ya jua na mtawala wa Dunia nzima, anatawala vitu vyote vya Duniani na Mbinguni na anakupa kalama ya uzima wa milele" anaweza kusikika Zumaridi akiwaambia watoto hao.
Baada ya kumaliza kuwapa somo hilo, Mfalme Zumaridi aliwaahidi watoto hao zawadi ya kuwapikia ubwabwa kwa kumfurahisha baada ya kuonyesha wakimtii na kumuabudu ipasavyo.
Lakini video hiyo iliwakera watumizi wengi wa mitandao na kumzomea vikali wengine wakifananisha mafunzo yake kama yale ya mchungaji mtata wa Kenya Paul Mackenzie ambaye anatuhumiwa kwa kuwahubiria waumini kuwa njia pekee ya kukutana na Mungu ni kujitesa njaa ya chakula na Maji.
Ikumbukwe mapema mwaka jana, Zumaridi na baadhi ya waumini wake walitiwa seli kwa kosa hilo na walikaa kwa kipindi cha miezi 11 na kuja kuachiwa baadae Februari mwaka huu.
Katika mahojiano na Millard Ayo siku chache baada ya kuachiliwa huru, Zumaridi alikiri kwamba ni yeye mtu pekee ambaye anafanya ziara za kwenda Mbinguni na kukutana na Mungu mara kwa mara, huku akijaribu kuwachorea walimwengu picha na taswira kuwa mbinguni watu wote ni weupe “kama Wachina”.