Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki kwa mara nyingine amekosoa na kukashifu vikali mauaji yaliyofanyika katika eneo la Shakahola chini ya itikadi potovu za imani zikiendeshwa na mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie.
Kindiki amesema kuwa mauaji hayo ni ukiukaji wa sheria za kulinda usalama na uhai na wananchi katika historia za taifa hili ambapo ameapa kuwachukulia hatua kali za kisheria wahubiri ambao hutumia maandiko matakatifu kuwalaghai raia.
“Mauaji ya Shakahola ni uvunjaji mbaya zaidi wa usalama katika historia ya nchi yetu. Ili kuzuia kurudiwa kwa janga hili, Serikali itasukuma kwa nguvu mageuzi ya kisheria kwa wahubiri wadanganyifu ambao hutumia vibaya maandiko kuwapotosha wafuasi wao na kuwafunza kupitia msimamo mkali wa kidini,” Kindiki aliposti katika mtandao wake wa Twitter.
Waziri Kindiki pia alisema kujitegemea itakuwa sehemu muhimu itakayowawezesha serikali kudhibiti na kufanyia mageuzi usimamizi katika mashirika ya kidini humu nchini, huku akidai kuwa utekelezaji wa sheria utaimarishwa ili kuzia kuenea kwa shughuli za kidini ambazo hazijulikani na ambazo zinajumuisha ufundishaji potovu wa watu wasio na hatia.
“Kujitegemea pia itakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa udhibiti na mageuzi katika usimamizi wa mashirika ya kidini. Utekelezaji wa sheria utaimarishwa ili kuzuia kuenea kwa shughuli za kidini ambazo hazijulikani ambazo zinajumuisha ufundishaji wa watu wasio na hatia,” Kindiki aliendelea.
Waziri huyo alisema kuwa ni wajibu wa viongozi katika serikali kuthibiti kuenea kwa dini potovu nchini pamoja na kutoa mielekeo inayopaswa kufuatwa na mashirika hayo. Alidai kuwa wahuni hawapaswi kupata nafasi katu ya kuendeleza imani imani potovu zinazolemaza maendeleo ya taifa.
Haya yanajiri wakati ambapo idadi ya miili ya watu waliofariki katika msitu huo ikiendelea kuongezeka kadri makaburi yanavyoendelea kufukuliwa.
Kindiki alisema kuwa haikosi kuna makaburi yalizikwa zaidi ya mwili mmoja ndani yake, ambapo alidai kuendesha shughuli ya ufukuzi hadi ibainike kiasi cha uharibifu ulioendeshwa na mhubiri Paul Mackenzie.