Mamlaka ya kudhibiti bei za kawi nchini EPRA imetangaza bei mpya za bidhaa za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta taa wiki mbili baada ya bei za awali.
Katika tangazo ambalo limetolewa jioni ya Julai 14 na EPRA, bei ya petroli imepungua kwa shilingi 0.85 huku bei ya dizeli ikisalia jinsi ilivyo nai le ya mafuta taa ikipungua kwa shilingi 3.96.
Ikumbukwe Julai mosi, EPRA waliwashtua Wakenya kwa kutangaza ongezeko la bei ya bidhaa hizo muhimu kwa bei ya juu Zaidi kuwahi kushuhidwa nchini.
Bei ya petroli iliongezeka kwa shilingi 13.49 huku ile ya dizeli ikiongezeka kwa shilingi 12.39 na mafuta taa ikaongezeka kwa shilingi 11.96.
Hii iliweka maisha ya wengi kuwa magumu kwani jijini Nairobi, Petroli ilianza kuuzwa kwa shilingi 195.53 kwa lita, dizeli ikiuzwa kwa shilingi 179.67 kwa lita na mafuta taa ikiuzwa kwa shilingi 173.44 kwa lita.
Hata hivyo, bei hizi mpya zilipata pingamizi kali kutoka kwa Wakenya wengi ambao walihisi ni mzigo mkubwa ambao umetwikwa mabegani mwao kutokana na kupitishwa kwa mswada wa fedha 2023.
Mwanaharakati ambaye pia ni seneta wa Busina Okiya Omtatah aliungana na chama cha mawakili LSK kuelekea mahakamani kupinga mswada huo.
Mahakama ya juu ilipiga breki mswada huo, uamuzi ambao pia ulidumishwa na mahakama ya rufaa na sasa kesi inaelekea katika mahakama ya upeo ambapo jaji mkuu Martha Koome anatarajiwa kuteuwa jopo na majaji watatu kusikiliza na kuamua hatima ya mswada huo uliotajwa na upinzani kama wa kumkandamiza mwananchi wa kawaida.
Katika mswada huo, ulikuwa na pendekezo la kupandisha ushuru wa kukadiria ubora wa bidhaa za kawi, VAT kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16, jambo ambalo lilizua mfumuko wa bei ya bidhaa hizo kuanzia Julai mosi, ambayo ni mwanzo wa mwaka moya wa kifedha.