Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya, Raila Odinga ameongoza kundi la Wakenya waliozungumziwa zaidi katika Bara la Afrika ndani ya mwezi Julai, huku Rais Ruto akishikilia nambari ya 25 katika orodha hiyo.
Kwa mujibu wa orodha iliyochapishwa na Afrika Social Charts, Kiongozi huyo wa chama cha ODM pia alishikilia nambari ya kwanza kwa watu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki waliozungumziwa sana katika mitandao ya kijamii barani.
Rais Ruto aliibuka nambari 25 naye naibu wake, Rigathi Gachagua akishikilia nafasi moja mbele yake.
Mchekeshaji maarufu Timothy Kimani almaarufu Njugush alitangazwa kama mtu wa 15 akiwa nambari ya pili ya Wakenya waliozungumziwa zaidi mitandaoni.
Orodha hiyo ilijumuisha washirika kutoka kote barani, huku nambari ya kwanza ikishikiliwa na Mnigeria Israel Adasanya na mlinda lango wa timu ya Inter Milan Andre Onana akiwa nambari ya pili. Mchezaji huyo amegonga vichwa vya habari kwa muda sasa huku mashabiki wa timu ya Epl, Manchester United wakiongojea kwa hamu kukamilishwa kwa usajili wake kwa mashetani hao wekundu wiki hii.
Baadhi ya Wakenya waliokuwepo kwenye orodha hiyo ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Sharon Barang’a, Njambi McGrath wakishikilia nambari ya 43,27,30 mtawalia.
Pia katika orodha hiyo palikuwepo na jina ya mchekeshaji anayekumbwa na utata katika taaluma yake na mahusiano, Crazy Kennar aliyeshikilia nambari 28. Wanamuziki Wakadinali pia walishikilia nambari ya 39.
Mchezaji wa zamani wa Kariobangi Sharks, Tyson Otieno ambaye hivi majuzi amehamia timu ya Kenya Police alikuwa ndiye mchezaji wa soka kutoka Kenya pekee ambaye alijumuishwa katika orodha hiyo akishikilia nambari ya mwisho ya 50.
Orodha hiyo ilijuimuishwa kutoka mitandao yote ya kijamii na kutumia uchambuzi wa Google kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 16 Julai.