Mjuzi na mchambuzi wa maswala ya kisiasa Mutahi Ngunyi amemwandikia rais Ruto ujumbe wenye ukakasi mwingi saa chache baada ya ripoti kuibuka kwamba ulinzi wa mama wa kwanza wa taifa, Ngina Kenyatta kudaiwa kuondolewa.
Kupitia ukurasa wa Twitter, Ngunyi alimtaka Ruto kutoruhusu siasa kuenda kinyume na matakwa ya ulinzi wa watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini ambao wanaonekana kupinga na kukosoa uongozi wake.
Ngunyi alisema kwamba Ruto ameondoa ulinzi wa Ngina na huenda majangili wakamshambulia lakini pia akamkumbusha kuwa hakuna tofuati kati yake na Uhuru Kenyatta kwani kesho kesho kutwa majangili hao watamwendea mamake, Sarah Ruto.
“Mpendwa Ruto: UMATI hawana akili. Leo WATAMVAMIA Mama Ngina huko Muthaiga. Kesho watamtafuta mama YAKO popote atakapokuwa. Hakuna TOFAUTI kati yako na Uhuru. Ukianzisha TREND hii, HAITASIMAMA. Pambana kama WANAUME na tuwaachie MAMA zetu. Tafadhali,” Mutahi alimtaka Ruto.
Ngunyi alisisitiza akimwambia Ruto kwamba adui si Mama Ngina bali adui ni watu ambao wanasukumwa na ugumu wa maisha na njaa pia, akimtaka kumtafuta Odinga na kufanya mazungumzo naye lakini kuwaacha kina mama kwa viongozi hao mbali na mihemko hii ya kisiasa.
“Kwa Ujumla: Adui SI Mama Ngina. Adui ni WATU. Ni rahisi KUZUNGUMZA na Raila, kuliko KUZUNGUMZA na watu WENYE HASIRA wakiongozwa na watu usiowajua. Usidhani kuwa UNAJUA. Mpendwa Ruto, UNAZINGATIA tatizo HALISI,” Ngunyi alisema.
Ulinzi wa Mama Ngina unadaiwa kuondolewa siku chache tu baada ya Ruto kumzomea vikali mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kwa kile aliashirika kwamba yeye ana mkono katika zogo la maandamano ya upinzani.
Upinzani umetangaza kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatano hii asubuhi kote chini kama njia moja ya kumshinikiza Ruto na uongozi wake kushuka chini na kuwasikiliza wananchi kuhusu mzigo mzito wa ushuru ambao umetwikwa mabegani mwao baada ya mswada wa fedha wa 2023 kupitishwa kama sheria mwezi mmoja uliopita.