Maandamano yamezuka katika kaunti ya vihiga kaunti ndogo ya Hamisi huku vijana wakiimba Ruto lazima aende kutawala hewani.
Wakiwa katika eneo la Gisambai waandamanaji walisema rais Ruto aliwadanganya. Mmoja wa waandamanaji alisema rais alipokuwa kwenye kampeni aliahidi kuwapa bodaboda na mama mboga maisha mapya ambayo hayajafikiwa.
"Rais aliahidi kupunguza gharama ya maisha, kupunguza bei za bidhaa za petroli lakini bado hatujaona hilo," mmoja wa waandamanaji alisema.
Maandamano hayo yalioitishwa na muungano wa Azimio yalianza siku ya Jumatano na yanatarajiwa kuendelea hadi siku ya Ijumaa. Kulingana na serikali maandamano Jumatano yalisababisha vifo vya watu wasiopungua sita kwa kupigwa risasi na wengine 30 kujeruhiwa katika maeneo tofauti.
Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa vifo hivyo viliripotiwa katika maeneo ya Nairobi, Wote, Nakuru na Kisumu huku kukiwa na hofu kuwa huenda idadi ya vifo itaongezeka.
Zaidi ya watu 30 wanauguza majeraha baada ya makabiliano na polisi. Wengi wa waathiriwa walipigwa risasi katika mitaa ya mabanda ya Nairobi, Nakuru, Kisumu na Makueni. Polisi walisema walikamata zaidi ya watu 300 kwa kushiriki maandamano hayo.
Watoto waliojipata katikati ya makabiliano hayo pia wanauguza majeraha katika hospitali mbali mbali.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema watu 300 walikamatwa Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na miji mingine ambapo polisi walikabiliana na waandamanaji.
Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na; Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga, kakake Peter Kamunya miongoni mwa wengine.
Njenga alikamatwa kutoka kwa nyumba ya babake huko Kiserian na zaidi ya maafisa 50 waliovamia boma la babake Jumatano usiku na kupelekwa mahali pasipojulikana.
Baada ya kukamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Babu Owino alipelekwa hadi kituo cha polisi cha Wanguru huko Kirinyaga na kuzuiliwa humo.