Watu watano kutoka familia moja eneobunge la Ganze kaunti ya Kilifi ambao walifariki kutokana na kula uyoga wenye sumu walizikwa wikendi iliyopita katika hafla ya mazishi iliyojawa majonzi, jitimai na simanzi tele.
Watano hao wote walikuwa ni watoto wa kati ya miaka 6 hadi 14 na walisemekana kula uyoga wenye sumu siku chache zilizopita.
Kulingana na taarifa hiyo iliyoripotiwa na runinga ya Citizen ambao walionesha hafla yqa mazishi hayo ikiendelea, watu walijawa na majonzi tele kuwaaga watoto hao katika makaburi matatu.
Ulaji wa uyoga wa sumu ulilaumiwa kwa uhaba wa chakula ambao umeshuhudiwa katika eneo hilo la Ganze ambapo wenyeji walisema hawakupata mavuno ya kutosheleza familia nyingi, hivyo kuwalazimu watoto kuingia vichakani kutafuta chakula.
Watano hao ni pamoja na Furaha Juma mwenye umri wa miaka 14, Mariam Juma wa miaka 9, Shariff Juma wa miaka 7, Mustafa Juma wa miaka 6 na binamu wao Eddie Juma wa miaka 9.
Watoto hao wote walikuwa wanasoma katika shule moja iitwajo Muungano Primary na walifariki katika tarehe tofauti kati ya Julai 22 hadi Julai 25 baada ya kuanza kulalamika maumivu ya tumbo Julai 21 baada ya kula uyoga wa sumu.
Juma Chalo alipoteza wanawe wanne kati ya wanane katika familia yake alishindwa kutembea wala kuzungumza.
Wenyeji wa eneo hilo walitoa wito kwa serikali kuanzisha mpango wa chakula angalau kwa watoto shuleni ili kuzuia visa vya watoto kwenda misituni kutafuta vyakula amabvyo vingine mwisho wa siku hugeuka kuwa sumu.