Katika miaka ya hivi karibuni, maeneo ya Gusii na Pwani ya Kenya haswa kaunti ya Kilifi kumekuwa na visa vya mauaji ya wakongwe wakituhumiwa kuwa wachawi.
Imetajwa kwamba wakongwe katika maeneo mengi wamekuwa wakionekana kama mzigo katika jamii huku mabadiliko mengi yakitokea na majukumu yao kuendelea kudidimika, wengi wanaona kama kuishi nao ni mzigo.
Hata hivyo, kuna baadhi ambao wamejitolea kuwatunza, wengine kwa kuanzisha vituo vya wakongwe ili kuwapa matunzo na upendo wanaohitaji wakati familia zao zinawatenga.
Katika eneo la Gusii, wakongwe wengi wamekuwa wakishambulia na kuuawa na jamii kwa kusingiziwa kuwa wachawi na sasa mashirika mbalimbali yamejitokeza kutoa wito kwa jamii hii kutowatenga au kuwaua wakongwe na badala yake kuwatunza.
Moja ya shirika hilo ni Ahadi Kenya ambao waliita kongamano katika eneobunge la Bobasi kama ilivyoripotiwa na runinga ya Citizen, wakilenga kuondoa dhana ya kuhusisha nywele za mvi na uchawi.
“Ni vibaya sana kwa mtu yeyote kunyoosha kidole chake kwa mkongwe mwenye umri wa miaka 80 au tisini na kumuita mchawi,” mmoja alisema katika kongamano hilo.
Kongamano hilo liliwarushia wakongwe tafrija la miziki ya kitamaduni, vyakula vizuri pamoja na zawadi zingine kama mablanketi na godoro za kulalia ili kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa.
“Upendo ni kitu cha maana sana katika dunia, ndio wenzetu wametuletea mikate, unga, blanketi na vitu vingine, tunasema ahsante,” mmoja wa wakongwe hao alisema kwa tabasamu pana kwenye panda la uso wake.