Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli amewasuta viongozi wa Azimio kwa kuandaa na kushiriki maandamano.
Akizungumza wakati wa ibada ya madhehebu mbalimbali mjini Bungoma Jumapili, Atwoli alisema Rais William Ruto alishinda uchaguzi wa Agosti 2022 licha ya muungano wa Azimio kuungwa mkono na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.
Alisema wanaofanya maandamano hawana ofisi za kurejea baada ya muda wa uchaguzi kupita, huku akiwataka wanaoshikilia wadhifa huo kuzingatia kazi zao.
“Mambo ya maandamano ni ya watu hawana ofisi. Wale watu walikuwa kwa Azimio akina Otuoma, Francis Atwoli, Ottichilo na wengine ambao walikuwa na ofisi wakati wa uchaguzi zilikwisha tulirudi kwa ofisi,” alisema.
Aliongeza;
“Wale wako kwa mambo ya maandamao; Kalonzo Musyoka hana ofisi, Martha Karua hana ofisi, mheshimiwa Wamalwa ndugu yetu hapa ofisini, Raila mwenyewe hana ofisi. Yule anaitwa Oparanya from my home has no office kwa hivyo maandamano muwachie watu wasio na ofisi. Wale walio na ofisi warudi kwa ofisi wafanye kazi,” aliongeza.