Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amewakashifu Wakenya wanaomkosoa kufuatia mahojiano yake na blogu moja ya humu nchini siku ya Jumatatu ambapo alitoka nje ya mada.
Katika taarifa yake Jumanne asubuhi, Salasya alibainisha kuwa alichaguliwa ili kuwakilisha eneo bunge lake na sio kuzungumzia mabadiliko ya hali ya anga.
Mbunge huyo wa muhula wa kwanza aliwashutumu wale wote wanaomkosoa na kuwataka pia wagombee nafasi za kuchaguliwa kuwa kama yeye.
"Wajinga wote hao wananikosoa kwenye twitter jinsi nilivyojibu kwenye #spm kuhusu #climatechange wakwende Uko na kizungu Yao wasimame kura pia wawe wabunge katika maeneo yao. siasa ni local wakwende na kizungu Yao. Sikuchaguliwa kuzungumzia mabadiliko ya tabianchi wajianga munisikie,” Salasya alijibu kwa sauti ya hasira.
Katika chapisho lingine, Mbunge huyo wa Mumias Mashariki aliwasasisha wafuasi wake kwamba kwa sasa yuko mjini Kisumu pamoja na wabunge wengine ili kujadili masuala yanayohusu sukari.
"Mambo na #climate siyafahamu achieni wanasayansi na wataalam .Watu wafwate maagizo yanatolewa kwenye #kicc," alisema.
Mbunge huyo kijana amekuwa akikosolewa sana katika saa chache zilizopita juu ya ufahamu wake duni wa mambo ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika video iliyofikia Radio Jambo, mbunge huyo aliulizwa jinsi anavyopigania mabadiliko ya tabianchi na iwapo ana mpango wa kusaidia nchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini hakuweza kutoa jibu linaloeleweka.
Wakenya walioona video hiyo mitandaoni walimkosoa, wakisema kwamba mtu wa hadhi yake anafaa kuwa ufahamu wa mada hiyo.
Salasya alikuwa miongoni mwa viongozi waliochaguliwa kuhudhuria Kongamano la Hali ya Hewa barani Afrika katika KICC.