Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amewajibu wanaomshambulia mitandaoni kufuatia mahojiano ya hivi majuzi kuhusu Tabianchi wakati wa kongamano la tabianchi lililofanyika Mjini Nairobi.
Katika mahojiano na SPM Buzz, mbunge huyo wa awamu ya kwanza katika bunge la kumi na tatu alisema;
“Mabadiliko ya hali ya hewa ni ya kweli kwa sababu ya ongezeko la joto duniani, yale yatakayo jadiliwa kwenye kongamano hili, ikiwa yatatekelezwa basi ni kwa manufaa ya nchi,”
Mbunge huyo aliongeza kuwa;
“Kama wabunge ambao tumechaguliwa kuwakilisha maeneo bunge, tunapigia upato sana swala la mazingira katika maeneo bunge yetu kwa kuwashauri watu waepuke kutumia kuni ili kutumia gesi ama jiko za kisasa ambazo hazitatatiza mazingira, tuko na mpango, na vijana wetu wako na mapendekezo ambayo tunadhamiria kuwasilisha bungeni ili wapate ufadhili wa kuyatekeleza,”
Baadaye mwanablogu, Pauline`Njoroge alitoa maoni kuhusiana na mahojiano ya Salasya akisema,:
“Najua hauko tayari kwa mazungumzo haya lakini kama nchi tunapaswa kuwacha kuchagua watu kwa sababu ya huruma na kuanza kuchagua watu wanaofaa kwa majukumu, kusema kweli Peter Salasya hafai kuwakilisha Mumias Mashariki,”
Mbunge huyo sasa amejitokeza kujieleza kwa kina kuhusiana na mahojiano hayo.
Kwenye kanda ya video aliyoachilia mitandaoni julai 6, Salasya alijieleza akisema kuwa, alikuwa amehudhuria kongamano hilo kwa hiari yake, kwani, yeye si mwanaharakati wa mazingira na kusema kwamba hafahamu mambo ya tabiainchi.
Salasya vilevile alijitetea akisema,
“Ni vigumu kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ya umaskini na jinsi watu wanvyoishi, na hivyo ndivyo nilivyosema,”
Aidha amedai kuwa alijaribu kutumia lugha ambayo inaleweka na kila mtu kando na wenzake wanaotumia kingereza tu.