Wakenya watalazimika kusubiri hadi Novemba 24 kujua hatma ya sheria ya fedha 2023/24.
Hii ni baada ya mahakama Kuu kusema kwamba itatoa uamuzi wake katika kesi dhidi ya Sheria hiyo Novemba 24.
Jopo la majaji watatu David Majanja, Christine Meoli na Lawrence Mugambi liliteuliwa na jaji mkuu Martha Koome kusikiza kesi iliyowasilishwa na seneta wa Busia Okiya Omutata na mashirika mengine yasio ya serikali kupinga sheria ya fedha 2023/24.
Vikao vya kusikiza mawasilisho ya pande zote vilikamilika siku ya Jumatano.
Uamuzi wa kesi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) anayedaiwa kupuuza amri ya mahakama katika kutekeleza sheria hiyo pia utatolewa Novemba 24.
Baadhi ya vipengele tata katika msuada huo ni makato ya 1.5% ya ujenzi wa nyumba kwa kila mfanyikazi, ushuru wa 16% wa ubora wa bidhaa kwa mafuta ya petroli na nyongeza ya kodi ya mapato kwa wafanyikazi wanaopata mshahara wa zaidi ya shilingi laki tano.