Idadi ya makaburi 21 katika eneobunge la Lari kaunti ya Kiambu yamefukuliwa na maiti kuondolewa ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopeperushwa katika runinga ya NTV, miili hiyo iliyokuwa imezikwa katika sehemu ambayo ilifaa kupita barabara ya Mau Mau yenye umbali wa kilomita 22 ilibidi iondolewe ili ujenzi wa barabara hiyo kufanyika.
Mwanakandarasi huyo alipata maagizo ya mahakama wakati wa serikali ya Uhuru Kenyatta ya kufukua miili ili kujenga Barabara ya Mau Mau yenye urefu wa kilomita 22.
“Tulipata agizo la mahakama mwaka jana wakati wa uongozi uliopita, kwa sasa katika sehemu ya kwanza ya barabara hii tuna makaburi 38, mwaka jana tulihamisha makaburi 5 na sasa tuko katika harakati za kuhamisha makaburi 33 yaliyosalia,” alisema msimamizi wa afya wa mradi huo.
Wakazi walisema walipogawiwa ardhi hiyo, hawakuwahi kutabiri mzozo uliopo ambapo wanalazimika kuchimba masanduku ya wanafamilia wao walioaga.
“Wakati tulipewa haya mashamba tulifikiria tu ni sehemu ya kawaida ambapo hakuna vile barabara ingepita kwenye mashamba yetu. Sasa ndio tunafukua haya makaburi ndio tuwaondolee kwa barabara waendelee na kazi,” mmoja wa wakaazi alisema.
Inaarifiwa kwamba wanakijii watakaoathirika kwa uhamisho wa makaburi ya wapendwa wap watafidiwa kiasi cha shilingi elfu 50 kwa kila kaburi.
“Vile walituambia tujitayarishe hakuna kitu walitufidia,” mama mmoja alisema.