Runinga ya Citizen imefanya ufichuzi jinsi baadhi ya Wakenya wakazi wa Moyale kaunti ya Marsabit kaskazini mwa Kenya wanavyofaidi pakubwa kutokana na petroli inayoingizwa nchini kwa njia ya magendo kutoka nchi jirani ya Ethiopia.
Kwa mujibu wa Makala hayo, petroli hiyo inaingizwa kutoka Ethiopia na kuuzwa vichochoroni kwa wakazi wa muji huo kwa shilingi 150 kwa lita kinyume na bei iliyoratibiwa na EPRA humu nchini ya wastani wa shilingi 220 kwa lita katika kaunti hiyo.
Mafuta hayo ya petroli yanauzwa kwa chupa za plastiki.
Makala hayo yalidai kwamba waendeshaji wa biashara hiyo wanavuka mpaka na kuingia nchini Ethiopia ambapo wanainunua bidhaa hiyo adimu kwa bei nafuu, mtungi wa lita 20 wakiupata kwa kati ya 1500 na 2800.
“Tunatumia tu haya mafuta ya kupima hayaishi haraka, hatutumii mafuta mengine. Uchumi umekuwa mbaya, bei ya mafuta ya Kenya iko juu na lakini Ethipoia iko rahisi na nafuu, kwa hiyo inatukalia rahisi kutumia hayo ya Ethiopia,” mhudumu wa bodaboda alisema.
Hali hiyo ya kila mhudumu wa chombo cha kutumia petroli kukimbilia petroli ya Ethiopia imeathiri pakubwa vituo vya petroli mjini Moyale Kenya kwa kuwa vimesalia mahame kila mmoja akikimbilia petroli nafuu ya Ethiopia.