Mwanamume mmoja na mwanawe ambao waliwatupia kinyesi cha binadamu maafisa wawili wa polisi nyumbani kwao katika mtaa wa Chokaa, eneo la Njiru, kaunti ya Nairobi wamekiri mashtaka ya kuzuia kukamatwa.
Kimathi mwenye umri wa miaka 57 na mwanawe Eric Jamal ,28, ambao pia wanaripotiwa kuwamwagia maji maafisa hao walikuwa wameshtakiwa kwa kuwazuia kutekeleza wajibu wao wakati walipofika nyumbani kwao mnamo Oktoba 8 kuwakamata kwa madai ya kuhifadhi bangi.
Wawili hao ambao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makadara, Irene Gichobi siku ya Alhamisi asubuhi pia walishtakiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya baada ya gramu 280 za bangi inayokadiriwa kuwa ya thamani ya shilingi 8,400 kupatikana nyumbani mwao.
Mahakama ilisikia kwamba maafisa hao wa polisi walikuwa wamevamia nyumba ya washukiwa hao baada ya kupokea ripoti za kijasusi kutoka kwa umma kwamba Jamal alikuwa akiuza bangi nyumbani kwake. Walipofika, walimkuta Jamal akiwa amelala, misokoto miwili ya bangi ikiwa kwenye meza yake na wakataka kumkamata.
Ni wakati huo ambapo mzee Kimathi aliingia ndani ya nyumba na kumshika afisa mmoja na kumfanya afiatue risasi hewani ili kumtishia. Kimathi hata hivyo aliondoka na kuchota kinyesi na maji ambazo aliwarushia maafisa hao huku akichochea umma dhidi yao.
Washukiwa hao wawili hata hivyo walikamatwa na kusindikizwa hadi kituo cha polisi baada ya bangi kupatikana chini ya kitanda chao.
Baada ya kukiri mashtaka dhidi yao, hakimu Gichobi aliagiza warudishwe rumande hadi Oktoba 24 wakati kesi dhidi yao itakapoendelea.