Taifa la Tanzania limepiga hatua kubwa kwa kuzindua kituo cha kwanza cha kufanyiwa uoasuaji wa kuongeza makalio kwa wanawake katika hospitali ya kitaifa ya Muhimbili nchini humo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka taifa hilo usini mwa Kenya, kituo hicho cha kufanya upasuaji wa kuongeza makalio na kurekebisha shepu ni cha kwanza kabisa na kitawafaa pakubwa watu wengi ambao wanasafiri kila uchao kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya upasuaji huo.
Upasuaji huo utahusisha kupunguza mafuta ya mwilini na kurekebisha maungo ikiwemo kupunguza au kuongeza ukubwa wa matiti na makalio, kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili, jarida moja lilisema.
Hayo yalisemwa Jumatano, Oktoba 10, 2023, na Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Dkt Eric Muhumba alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu upasuaji huo.
Dkt Muhumba alisema upasuaji huo utafanywa na wataalamu wa Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa upasuaji wa kupunguza uzito na upasuaji rekebishi kutoka India, Dkt Mohit Bhandari pamoja na Taasisi ya Afya ya MedINCREDI.
Alisema huduma hizo za kupunguza uzito zinafanyika kwa kupunguza nafasi ya kuhifadhi chakula kwa kushona sehemu ya eneo la tumbo kitu kitakachosababisha mtu kutumia kiasi kidogo cha chakula hivyo kupunguza uzito.
Dkt Muhumba alieleza kuwa katika kutoa huduma hizo, watatumia njia ya kisasa ambayo haitahusisha upasuaji ambapo watatumia kifaa maalumu kiitwacho endoskopia kuingia katika tumbo na kupunguza nafasi ya tumbo la chakula.
“Upasuaji huu utafanyika kwa bei nafuu sana ukilinganisha na endapo mtu angeenda kutafuta huduma hizi nje ya nchi, hivyo tumeamua kuwasogezea wananchi huduma hizi na kuwapunguzia usumbufu wa wananchi kusafiri nje ya nchi kutafuta huduma hizi,” Dkt Muhumba alinukuliwa.
Sambamba na huduma hizo Dkt Muhumba aliongeza kuwa huduma rekebishi itahusisha kurekebisha kwa kupunguza mafuta na kurekebisha sehemu ya mwili mfano kupunguza au kuongeza ukubwa wa matiti, nyama kwenye mikono na sehemu nyingine mbalimbali za mwili.