Mshauri wa Rais William Ruto kuhusu masuala ya kiuchumi David Ndii amemchana Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja baada ya kundi la maafisa wa kaunti, almaarufu kanjos kunaswa kwenye kamera wakiharibu na kunasa mikokoteni ya wachuuzi wa mayai na smokies.
Katika taarifa yake, Ndii aliikashifu serikali ya Sakaja akiishutumu kwa kutokuwa rafiki kwa haslas.
Mchumi huyo pia alibainisha kuwa hapo awali aliwahi kutoa maonyo kadhaa kwa Gavana huyo kuhusu mfumo wake wa uongozi, na kuongeza kuwa licha ya wito huo wa mara kwa mara, mkuu huyo wa kaunti alishindwa kuzingatia ushauri wake.
"Uongozi wa Kaunti ya Nairobi sio rafiki kwa haslas. Ndio maana naendelea kumshawishi Johnson Sakaja. Sakaja anaendesha jukwaa la "kuagiza". Mpango wake ulikuwa wa kuweka wachuuzi sokoni. Wachuuzi wa mitaani wako mitaani kwa sababu huko ndiko wateja," Ndii alisema katika taarifa yake.
Kulingana na mwanauchumi huyo, sehemu kubwa ya Wilaya ya Biashara ya Kati ya Nairobi (CBD) inahitaji kupitishwa kwa miguu na kufanywa kuwa rafiki wa mitaani.
Ndii zaidi alichapisha picha za manifesto ya awali ya Sakaja ambapo gavana aliorodhesha mambo kadhaa ambayo angefanya ili kuboresha maisha ya wakazi wa Kaunti ya Nairobi.
Kauli ya Ndii ilijiri kufuatia malalamishi ya wafanyabiashara wa Nairobi baada ya mikokoteni yao kuharibiwa na maafisa wa Kaunti ya Nairobi.
Wakenya walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuelezea kukerwa kwao baada ya picha zinazoonyesha jinsi hali nzima ilivyoanza kusambaa mitandaoni.
Picha hizo zilionyesha smkies na mayai ya kuchemsha yakiwa yametapakaa kando ya barabara huku askari wa kaunti wakivuta toroli nyingine.