Magavana wawili wa kike wa chama tawala cha UDA wameahidi kumuunga mkono Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ambaye anakodolea macho shoka la kung'atuliwa mamlakani.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X Gavana wa Nakuru Susan Kihika alimshauri Gavana wa meru aliyetimuliwa kuongeza kilio chake na kumtazamia Mungu.
"Dada yangu mpendwa Gavana Kawira, weka mawazo yako yote juu kwa mwenyenzi Mungu na ujue hauko peke yako, nasimama nawe," alisema.
Geukia maombi, Kihika alisema kwamba anaomba mwenzake wa Meru atashinda majaribu haya yote na atajitokeza akiwa na nguvu na mshindi.
"Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili,na kukupa amani,Utakuwa heri dada yangu",aliongeza.
Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa Baraza la magavana ambaye pia ni Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru alimshauri Kawira kumgeukia Mungu katika kipindi hiki kigumu.
"Asiye kuwa na wake ana Mungu... nasimama nawe dada yangu Gavana Kawira Mwangaza,Ni giza kuu kabla ya mapambazuko,angalia Milima ambapo msaada wako unatoka.. Kuna Mungu Mbinguni," alisema.
Gavana Mwangaza Jumatano alitimuliwa kwa kauli moja na Bunge la Kaunti ya Meru baada ya hoja ya kumbandua mamlakani kuungwa mkono na wakilishi wadi 59 waliokuwepo Bungeni.