Wakazi wa mkoa wa Iringa nchini Tanzania wamepigwa na butwaa baada ya mwanamume mmoja aliyetambulika kwa jina Goodluck Mgovano mwenye umri wa miaka 33 kudaiwa kumuua mwanawe kwa Kamba za viatu kisha kurekodi tukio zima na kupiga picha ya selfie na maiti.
Kwa mujibu wa taarifa kupitia YouTube ya runinga ya Global TV Online, Mgovano alimnyonga mwanawe Alvin Mgovano mweney umri wa miaka 4 na baadae kabla ya kutoweka akaacha ujumbe wa maandishi kutoa maelekezo kuhusu ni wapi mtoto huyo atazikwa.
Kwa mujibu ya wakazi waliopigwa na butwaa, walisema kwamba mwanzoni walipomkuta mtoto hoi bin taabani kitandani, walidhani amekula sumu na wakachukua maziwa kumnywesha ili kukanya sumu.
Baadae waliona hali ya mtoto ilizidi kuwa mbaya na walipomkimbiza hospitalini ndipo madaktari walibaini kwamba alishafariki kitambo kwa kunyongwa.
Hapo ndio walirudi nyumbani na kupekua wakapata barua ya mtuhumiwa huyo ikielezea chanzo cha mauaji hayo lakini pia maelekezo ya ni wapi kaburi lichachimbwa.
“Simu yake yenye picha na video aliiacha hapohapo nyumbani na kwa sasa ipo mikononi mwa Polisi”
Mtuhumiwa aliacha ujumbe uliosema “Chanzo cha mauaji haya ni ugomvi uliotokea kati yangu Mimi na Mke wangu mnamo Oktoba 6, 2023 na mimi naenda kujiua na nataka mimi na Mwanangu tuzikwe Kijiji cha Itendulinyi”
Diwani wa Kata ya Mlandege, Jackson Chaula alinukuliwa na Global Tv Online akisema Mtuhumiwa alikuwa anafanya kazi ya ubebaji mizigo katika magari lakini hakuwa na shida yeyote, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa Alfred Mwakalebela amekiri kupokea mwili huo na kusema mwili huo ulikuwa na makovu ya shingoni.