Mahakama kuu ya Uganda imemhukumu mtu mmoja kifungo cha miaka 52 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto wa miaka mitano na kumtoa kafara, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.
Hakimu David Batema alimhukumu Hassan Kafudde kifungo cha miaka 52 jela pamoja na Issa Muyita, baba wa marehemu aliyehukumiwa miaka 25 kwa kumuua Juma Muyita, 5 ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Mirembe Junior iliyoko Kawempe mwaka 2017.
Katika uamuzi wake, Jaji Batema alibainisha kuwa adhabu hiyo inapaswa kuwa kizuizi kwa wahalifu wengine.
Kufuatia uamuzi huo, mawakili wa haki za mtoto waliohudhuria mahakamani waliipongeza mahakama kwa uamuzi huo.
Akihutubia wanahabari, msemaji wa DPP Jackline Okui alikaribisha hukumu hiyo ambayo alisema itasaidia kutenda haki.
Pia alitoa wito kwa wazazi kujiepusha na tabia ya kuwatoa watoto wao wenyewe ili kujipatia mali, akibainisha kuwa tabia hiyo imekithiri katika kitongoji cha Busoga.