Shirika la afya duniani WHO limeielezea hospitali ya Al Shifa kuwa inageuka kuwa kile ilichokitaja makaburi.
Msemaji wa WHO Christian Lindmeier amesema takriban watu mia sita wamekwama ndani ya hospitali hiyo na miili ya watu inarundikana ndani na nje ya hospitali hiyo kubwa zaidi Gaza ambayo Israel hairuhusu isafirishwe kuzikwa au kuhamishwa kwa vyumba vya kuhifadhia maiti.
Madaktari wa hospitali hiyo wanaonya karibu shughuli zote zimekwama, mbwa wameanza kuingia hospitalini humo kula maiti, wagonjwa wa figo wakishindwa kupata matibabu maalum na maisha ya watoto njiti yakiwa hatarini kwani umeme umekatwa.
Dkt Mohamed Abu Selmia aliambia BBC kwamba kwa vile mamlaka ya Israel bado haijatoa kibali kwa miili iliyoharibika kuondolewa hospitalini kuzikwa, mbwa sasa wameingia katika uwanja wa hospitali na kuanza kula maiti hizo.
Mark Regev, mshauri mkuu wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema Israel ilikuwa ikitoa "suluhu la vitendo" kuwahamisha watoto hao wachanga na kuwashutumu Hamas kwa kutokubali mapendekezo.
Pamoja na Al-Shifa, hospitali nyingine katika Ukanda wa Gaza zimeripoti masuala yaliyoenea, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa na nguvu kwa sababu ya mapigano na vikwazo vinavyotekelezwa na Israeli katika eneo hilo tangu Hamas ilipoanzisha mashambulizi yake kwa Israeli tarehe 7 Oktoba.