Mfanyibiashara aliyezingirwa na utata mwingi, Bi Anne Njeri Njoroge amethibitisha kuwa ni kweli mama yake hafahamu utajiri wake halisi.
Bi Pauline Wanjiru Njoroge, mnamo wiki jana, alieleza mshtuko wake baada ya binti yake kuhusishwa na mafuta ya thamani ya Ksh17 bilioni ambayo yamezuiliwa katika bandari ya Mombasa, akibainisha kuwa kwa zaidi ya mwezi mmoja hakuwahi kufahamu kuwa bintiye ni tajiri kiasi hicho.
Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen katika eneo lililofichwa, Anne Njeri alithibitisha madai ya mamake lakini akasisitiza kuwa anafahamu yeye ni mfanyabiashara.
"Mama hajui pesa yangu ni kiasi gani, anajua mimi ni mfanyibiashara, anajua hilo," alisema.
Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 55 alibainisha kuwa sio kila kitu kinachopaswa kufichuliwa.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na Nation, Bi Pauline Wanjiru alifichua kuwa bintiye hajamtembelea kwa miaka sita iliyopita, akifichua kuwa mazungumzo yake ya mwisho na Njeri mwenye umri wa miaka 55 yalikuwa kwenye simu takriban miezi minne iliyopita.
“Kwa kawaida huwa tunazungumza kwa simu inapobidi, nimekuwa nikiomba siku moja anitembelee, mara ya mwisho alikuwa hapa ni zaidi ya miaka mitano iliyopita, karibu miaka sita sasa ananiambia amekuwa na shughuli nyingi na niliacha kumuuliza ni lini atakuja kunitembelea," Wanjiru aliambia Nation.
Alizungumza akiwa nyumbani kwake kijijini Kianjege, Kaunti ya Kiambu.
"Ningependa kukutana na binti yangu ambaye unaniuliza," alisema.
Mjane huyo alifichua kuwa bintiye aliacha shule akiwa kidato cha kwanza na akabainisha kuwa hafahamu kazi halisi anayofanya siku hizi.
Hata hivyo, aliweka wazi kuwa mfanyibiashara huyo amekuwa akimsaidia kifedha mara kwa mara wakati anapohitaji.
“Anasaidia pale anapoweza na sina lolote la kibinafsi dhidi yake, ni pesa zake na hata sijui ni tajiri au la, ninachojua ananiambia anafanya biashara Dubai na Kenya, lakini mimi. siwezi kusema haswa anafanya kazi gani," Wanjiru alisema.