Watu 10 walikamatwa walipokuwa wakielekea katika Mahakama ya Nakuru kusikiza kwa kesi dhidi ya Maina Njenga.
Washukiwa wanne ambao walipata fursa ya angalau kupata kikombe cha chai baada ya kikao hicho kuhairishwa pia hawakuingia mahakamani baada ya kuzuiliwa kuingia.
Kesi hiyo ilikosa kuanza jinsi ilivyokuwa imeratibiwa baada ya timu ya utetezi kupinga uwepo wa polisi kwa wingi katika mahakama hiyo.
Hii ni baada ya mahakama kuruhusu upande wa utetezi na upande wa mashtaka kufanya mipango na kuruhusu watu mahususi kuingia ndani ya jengo hilo baada ya kudai kuwa jengo hilo halina uwezo wa kuwaruhusu watu wengi kuhudhuria vikao.
Wakili Ndegwa Njiru alisema ni makosa kwa polisi waliojihami kufunga barabara zote zinazoelekea katika Mahakama ya Nakuru kwa nia ya kuwazuia wananchi.
Alitishia kuwa upande wa utetezi utafanya maandamano ikiwa marafiki na jamaa wa washtakiwa 12 hawataruhusiwa kuhudhuria kikao cha mahakama akiongeza kuwa Kenya si taifa la polisi.
Alimwambia Hakimu Mkuu Kipkurui Kibelion kumwita Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru na kumwamuru kuwatoa maafisa hao wa polisi karibu na Mahakama ya Nakuru.
“Hata mawakili hawaruhusiwi kortini kabla ya kuonyesha vitambulisho ili kuthibitisha kuwa wao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria wa Kenya,” alisema.
Maoni yake yaliungwa mkono na Mawakili Evanson Ondiek na Olaly Cheche waliosema umma una haki ya kushuhudia utekelezaji wa haki.
"Polisi wanamchukulia kila mtu kama mwanachama wa Mungiki na hatujui ni nini kilichangia uamuzi wao," Ondiek alisema.
Aliishutumu Serikali kwa kutumia polisi kuwatisha watuhumiwa na jamaa zao.
Kiongozi wa mashtaka Wycliffe Omwenga alipuuzilia mbali maombi hayo kwa upande wa utetezi akisema kuwa mahakama hiyo ina uwezo wa kuwaruhusu watu wachache kuhudhuria vikao.
Alidai kuwa shahidi alizirai siku ya Jumatatu kutokana na msongamano katika chumba cha mahakama.
Hakimu Kibelion alibainisha kuwa ingawa mahakama haiwezi kuchukua kila mtu, upande wa mashtaka na upande wa utetezi unaweza kujadili nani wa kuruhusiwa kuingia.