Mfuasi maarufu wa Raila Odinga Nuru Okanga hivi majuzi alifichua maelezo kuhusu maisha yake ya utotoni na hali iliyomfanya aache shule zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Kwenye mazungumzo na runinga ya NTV mnamo Alhamisi, Novemba 23,kufuatia kuchapishwa kwa matokeo ya mtihani wa Shule ya Msingi ya Kenya (KCPE) 2023, Okanga alisema aliacha shule katika darasa la tatu kutokana na kifo cha babake.
“Niliachia darasa la tatu. Baba yangu alifariki nilipokuwa mdogo sana, naye alikuwa ameoa wake wengi. Tulikuwa watoto wengi, na mama yangu hangeweza kutusomesha na kutupatia chakula kwa wakati mmoja,” alisema Okanga mwenye umri wa miaka 32
Licha ya umri wake mdogo wakati huo, Okanga anasema, alikuwa mtoto mchangamfu, na kuondoka kwake shuleni kulimuathiri sana mwalimu mkuu wa shule, ambaye hata aliishia kumwaga machozi.
Alieleza kuwa alitoa sababu za kuacha shule kwa mkuu wa shule akiomba msaada, lakini kutokana na familia yake kuwa kubwa, msaada ulikuwa mdogo.
“Nilipofika darasa la tatu, ni sare ya shule na vitabu vilivyonifanya niache shule. Nilifaulu shuleni; Nimekuwa mwerevu tangu zamani. Nilipoacha shule, mwalimu mkuu alilia kwa uchungu,” alisimulia.
Ingawa ripoti zilizoenea zinaonyesha kuwa Okanga alifanya mtihani wa KCPE wa 2023 na kupata alama 401 kati ya 500,ripoti hizi, hata hivyo, bado hazijathibitishwa.
Anasema alifanyia mitihani hiyo katika Shule ya Msingi ya Mumias Muslim kaunti ya Kakamega na na amesalia na msimamo dhabiti wa matokeo hayo.
Okanga ameshabikiwa na watu wengi mitandaoni ambao wamempongeza kutokana na habari hizo zinazoenea.
Mbunge wa Embakasi mashariki Babu owino,alichapisha mitandaoni na kusema kuwa amejitolea kusimamia masomo ya sekondari ya Nuru Okanga.
Aidha Okanga alifichua kuwa Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alimzawadi vinono baada ya kuandikisha matokeo hayo.